Waziri wa zamani wa biashara wa Ivory Coast, Jean-Louis Billon, amekubali kushindwa na Rais aliyepo madarakani, Alassane Ouattara, katika uchaguzi wa urais wa taifa hilo, kufuatia matokeo ya awali yanayoonyesha Ouattara akiongoza katika kura zilizohesabiwa.

Billon alikuwa miongoni mwa wagombea wanne wa upinzani waliompinga Ouattara, ambaye ana umri wa miaka 83 na ni afisa wa zamani wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ambaye anawania muhula wa nne madarakani.

Billon hakufanikiwa kupata uungwaji mkono wa chama kikuu cha upinzani, PDCI, kinachoongozwa na Tidjane Thiam , aliyekuwa mkuu wa benki ya Credit Suisse, ambaye alizuiwa kugombea.

Tume Huru ya Uchaguzi ya nchi hiyo ilianza kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi wa Jumamosi kupitia televisheni ya taifa siku ya Jumapili.

Takriban raia milioni tisa wa Ivory Coast walikuwa na haki ya kupiga kura katika uchaguzi uliogubikwa na mgawanyiko wa upinzani, hali iliyozidishwa na kuenguliwa kwa wagombea wawili wakuu.

Wapinzani wakuu wa Ouattara ,  Rais wa zamani Laurent Gbagbo na Thiam,  walizuiwa kugombea; Gbagbo kutokana na kupatikana na hatua ya jinai, na Thiam kwa sababu ya kuchukua uraia wa Ufaransa.

Hali hiyo ilisababisha maandamano kabla ya uchaguzi na miito kutoka kwa baadhi ya makundi kutaka uchaguzi ususiwe.

Ingawa idadi rasmi ya waliojitokeza kupiga kura haijatangazwa, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, Ibrahime Coulibaly-Kuibiert, awali alikadiria kuwa ni takriban asilimia 50.

Uchaguzi wa Jumamosi ulifanana na ule wa mwaka 2020, ambapo Ouattara alipata asilimia 94 ya kura huku idadi ya wapiga kura ikiwa kidogo zaidi ya asilimia 50, katika uchaguzi uliosusiwa na idadi kubwa ya wapinzani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *