Dar es Salaam. Mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalim, amehitimisha kampeni za chama hicho huku akiwashukuru Watanzania namna walivyompokea katika maeneo yote ya nchi alipopita.

Mwalim alifunga kampeni hizo leo Jumatatu Oktoba 27, 2025 katika mkutano mkubwa uliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Tabata jijini Dar es Salaam.

Mgombe huyo amesema ametembea mikoa yote kasoro Zanzibar, kutokana na masuala ya lojistiki kutokaa vizuri.

Mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalim

“Nashukuru kote huko nilikotembea Watanzania wamenipokea kijana wao vizuri, sina cha kuwalipa zaidi ya kuwashukuru na kuwaombea siku ya kupiga kura muende mkaniamini kwa kuwa nawahakikishia nchi itabaki salama na nitaendelea kulinda udugu wetu wa asili.

“Pia nawahakikishia Watanzania mkinipa nchi hakuna atakayeumia, nitaendelea kudumisha umoja na mshikamano wetu na wala msinipime kwa umri wangu, kwani hata Baba wa Taifa aliongoza nchi hii akiwa na miaka 39 lakini ndio aliyejenga nchi hii leo tunayoikalia,” amesema Mwalim.

Akitoa tathimini yake katika kampeni alizofanya, Mwalimu amesema kote alipopita watu wanalia maisha magumu.

“Watu wanalia, Kusini, Lindi na Mtwara wakulima wa korosho wanalia, Shinyanga wanalia na pamba, Manyara wanalia na ufuta na alizeti, Dodoma wanalia na alizeti na zabibu,Morogoro na mpunga. Kifupi nchi inalia kila kona gharama za uzalishaji ni kubwa,”amesema Mwalim.

Kwa upande wa wafugaji amesema wanalia kwa kuwa watumwa kwenye nchi yao katika ardhi ambayo ni takatifu waliojaliwa na Mungu.

“Nimekwenda Katavi, Kagera, Lindi wote wanalia huko, kwani kila ardhi leo inachukuliwa kama ardhi oevu, hifadhi na hivyo kuhaha kukosa malisho.

Kwa upande wa wafanyabiashara amesema wanalalamika kodi na tozo ni nyingi jambo linalochangia kuua mitaji yao.

Mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalim

Kwa upande wa vijana amesema wanalia hakuna ajira, huku maisha yao yamekuwa kubeti na bodaboda na kuwa watu wa kubadilisha chaneli huku mkeka ukienda.

Kwenye afya ameeleza kuwa amekutana na wakina mama wanalia, wanalipisha kodi kwa watoto, huku wakiwa wanalazwa wazazi wanne kwenye kitanda kimoja jambo ambalo kwenye uongozi wake hatolikubali.

Katika hitimisho lake, amewanadi wagombea wote wa ubunge wa Chaumma wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo aliwaomba wananchi wawachague ili akapate wasaidizi wa kuongoza nchi kwa kuwa wote ni majembe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *