
Kundi la wanagmbo wa Kikurdi la PKK limetangaza rasmi uamuzi wake wa kuondoa wapiganaji wake wote nchini Uturuki kuelekea kaskazini mwa Iraq, kama sehemu ya mchakato wa kuweka chini silaha.
Kundi hilo limekuwa likiendesha uasi nchini Uturuki tangu miaka ya 1980, ambao umeosababisha vifo vya maelfu ya watu.
Tangazo hilo limetolewa katika hafla iliyofanyika katika Milima Qandil kaskazini mwa Iraq jana Jumapili, ambapo taarifa iliyosomwa na msemaji wa kundi la PKK ilisisitiza kuwa wapiganaji wa kundi hilo wamedhamiria kuanza “maisha huru, ya kidemokrasia na ya kindugu” kwa kuondoa wapiganaji wake wote nchini Uturuki.
Kunidi la PKK pia limeiomba serikali ya Uturuki kufanikisha kipindi cha mpito kuelekea katika siasa za kidemokrasia kwa kutunga sheria jumuishi. PKK imesema imedhamiria kwa dhati kuona mchakato wa kuweka chini silaha unatekelezwa.
Zagros Hiwa, msemaji wa kundi la wapiganaji wa Kikurdi la PKK amesema wako katika njia ya kutekeleza mradi wa amani wa kiongozi wao, Abdullah Ocalan na kwamba upande mwingine yaani serikali ya Uturuki unapasa kufanya mabadiliko ya kisiasa na kutayarisha mazingira yanayofaa ili mradi huo uweze kutekelezwa.
Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki amepongeza hatua hiyo na kuitaja kuwa muhimu kwa ajili ya kudumisha amani na undugu nchini humo.