Hii ni rekodi mpya kwani tangu Tanzania ianze kuingiza timu nne katika michuano ya CAF ngazi ya klabu msimu wa 2019–20, haijawahi kutokea timu zote za Bara zikafuzu hatua ya makundi, safari hii rekodi mpya imewekwa.

Tayari tumeshuhudia mara tatu mfululizo wawakilishi wetu wakicheza makundi ndani ya msimu mmo-ja, Simba na Yanga, lakini hakuna zaidi ya hapo.

Ilikuwa 2022-2023, Simba ikicheza makundi Ligi ya Mabingwa na kuishia robo fainali, Yanga ikawa upande wa Kombe la Shirikisho ikaenda hadi fainali, kisha 2023-2024 zote zilikuwa makundi Ligi ya Ma-bingwa na kuishia robo fainali, ndipo 2024-2025 Simba ikacheza makundi Kombe la Shirikisho na Yanga Ligi ya Mabingwa. Msimu huo Yanga iliishia makundi na Simba ikacheza fainali Kombe la Shirikisho.

Azam, Yanga na Singida Black Stars zilianza kutangulia, ikiisubiri Simba jana iliyokuwa na kazi ya kumal-izia baada ya ugeni kuuwasha moto ikiichapa Nsingizini mabao 3-0.

Kwa timu zote hizo kuingia makundi, ni rekodi mpya imewekwa hali inayofanya soka letu kuzidi kukua siku hadi siku.

YANGA INAIFUKUZIA SIMBA

Kitendo cha Yanga kufuzu hatua ya makundi, imeifanya kufika hatua hiyo ya michuano ya CAF kwa ma-ra ya sita ndani ya miaka kumi, ikiifukuzia Simba ambayo jana nayo ilikuwa na kibarua cha kurudiana na Nsingizini Hotspurs.

Kabla ya jana, Simba ilikuwa imefuzu makundi ya michuano ya CAF mara sita katika kipindi hicho, huku tano ikiwa mfululizo. Yanga yenyewe imefuzu mara nne mfululizo.

Rekodi zinaonyesha, Simba kabla ya jana kurudiana na Nsingizini ikiwa na mtaji wa mabao 3-0 ilioupata ugenini, imecheza makundi mara sita, Ligi ya Mabingwa (4) na Shirikisho (2).

Ubabe wa Simba ulianzia Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018-2019, kisha ikarudia tena katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2020–2021, ambapo kuanzia hapo ikawa inafuzu mfululizo kunako michuano ya CAF.

Msimu wa 2021-2022, haikufanya vizuri Ligi ya Mabingwa, ikaangukia Kombe la Shirikisho Afrika makundi.

Ikarejea tena Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2022–2023 na 2023–2024, kisha msimu uliopita 2024-2025 katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Mara zote ambazo Simba imefuzu makundi, imefika robo fainali, huku 2024-2025 ikicheza fainali.

Yanga mwaka 2016 ilicheza hatua ya makundi Kombe la Shirikisho, ilifanikiwa kwa kuiondosha Sagrada Esperança kwa jumla ya mabao 2-1. Ikapangwa Kundi A, ikamaliza mkiani na pointi nne. TP Mazembe iliongoza na pointi (13) ikifuatiwa na MO Bejaia (8) kisha Medeama (8), mabao yakawatofautisha. Wakati huo kulikuwa na makundi mawili pekee.

Ikapita miaka miwili, kisha mwaka 2018, Yanga ikacheza tena hatua ya makundi, ikaburuza mkia. Kum-buka ilifuzu makundi kwa kuitoa Welayta Dicha ikiifunga jumla ya mabao 2–1.

Ikapangwa Kundi D, Yanga ilimaliza tena mkiani na pointi nne. Kinara USM Alger pointi 11, Rayon Sports (9) kisha Gor Mahia (8).

Msimu wa 2022–2023 utabaki wa kukumbukwa kwa Yanga baada ya kucheza fainali ya Kombe la Shiriki-sho Afrika. Hiyo ilitokana na kutolewa Ligi ya Mabingwa, ikaangukia mtoano Shirikisho, ikaitoa Club Africain kwa bao 1–0.

Ikapangwa Kundi D, ikamaliza kinara na pointi 13, ikifuatiwa na US Monastir (13), Real Bamako (5) na TP Mazembe (3).

Kutoka hapo, Yanga imecheza makundi mfululizo upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya awali kucheza Kombe la Shirikisho.

Msimu wa 2023-2024, katika harakati za kufuzu makundi, iliitoa Al Merrikh kwa jumla ya mabao 3–0.

Hatua ya makundi ikaangukia Kundi D, ikamaliza nafasi ya pili na pointi nane nyuma ya vinara Al Ahly (12). CR Belouizdad nayo ilikusanya pointi nane, Medeama ikaburuza mkiani na pointi nne. Msimu huo Yanga ikakwamia robo fainali.

Msimu wa 2024-2025, Yanga iliitoa CBE kwa jumla ya mabao 7–0, ikafuzu makundi, ikapangwa Kundi A, Yanga ilimaliza nafasi ya tatu nyuma ya kinara Al Hilal iliyokusanya pointi 10 na MC Alger (9). Mkiani ilikuwa TP Mazembe na poonti tano.

Safari hii msimu wa 2025-2026, Yanga imeitoa Silver Strikers kwa jumla ya mabao 2-1, inasubiri droo ita-kayochezeshwa Novemba 3, 2025 kufahamu itapangwa kundi gani.

MASTA GAMONDI

Kufuzu kwa Singida Black Stars, kuna mambo mawili. Kwanza klabu hiyo kuandika rekodi kama ya Na-mungo iliyoiweka msimu wa 2020-2021 katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Ipo hivi; kabla ya msimu huu, ilikuwa ukiitoa Simba na Yanga zenye rekodi nzuri ya kucheza hatua ya makundi ya michuano ya CAF, kulikuwa hakuna klabu nyingine ya Tanzania tangu mwaka 2004 ilipoan-zishwa Kombe la Shirikisho Afrika iliyowahi kucheza hatua hiyo zaidi ya Namungo.

Kombe la Shirikisho Afrika, ni michuano iliyoanzishwa mwaka 2004 baada ya CAF kuyaunganisha mashindano mawili, African Cup Winners’ Cup yaliyoanzishwa mwaka 1975 na CAF Cup ya mwaka 1992, ndipo ikazaliwa yenyewe.

Singida Black Stars chini ya Gamondi imeifikia rekodi ya Namungo ya msimu wa 2020–2021 ambapo ilishiriki Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza na kufika hadi makundi licha ya kwamba hai-kuendelea zaidi ya hapo ikimaliza mkiani bila pointi.

Timu za Tanzania ambazo zimeshiriki michuano hiyo mbali na Simba na Yanga ni KMC (2019–2020), Mtibwa Sugar (2018-2019), Biashara United (2021–2022), Geita Gold (2022-2023), Singida Fountain Gate (2023-2024), Coastal Union (2024-2025), ambazo hazikutoboa. Ilikuwepo na Azam iliyowahi kushiriki mara nane kabla ya msimu huu kuvunja mwiko.

Ushindi wa mabao 3-1 nyumbani dhidi ya Flambeau du Centre, umefanikisha rekodi hiyo kwa Singida Black Stars.

Jambo lingine, Gamondi naye ameweka rekodi yake ya kuzifikisha timu mbili tofauti za Tanzania hatua ya makundi ya CAF kwa misimu mitatu mfululizo.

Awali alifanya hivyo mara mbili akiwa Yanga, aliifikisha timu hiyo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku moja akienda nayo hadi robo fainali 2023-2024, lakini ile ya 2024-2025, alisitishiwa mkataba ikiwa ni siku kadhaa tangu afuzu nayo makundi.

Katika kufuzu kwa Singida Black Stars, Clatous Chama amehusika kwa asilimia kubwa, wakati timu hiyo ikifuzu kwa jumla ya mabao 4-2, amefunga mabao mawili. Kwanza katika sare ya ugenini 1-1, kisha aka-funga bao la kuiweka mbele timu hiyo kabla ya Diomande kupigilia msumari wa mwisho na matokeo kuwa 3-1, juzi pale Azam Complex.

Kabla ya hapo, Chama pia mechi ya ugenini hatua ya awali dhidi ya Rayon, alitoa asisti ya bao lililo-fungwa na Marouf Tchakei, Singida iliposhinda 1-0.

IBENGE ALIVYOUTAFUNA MFUPA ULIOWASHINDA OMOG, LWANDAMINA

Misimu 10 ya Azam kushiriki michuano ya CAF ilikuwa na hadithi ya kufanana, kama sio kutolewa hatua ya awali, basi inaishia hatua ya pili, kucheza makundi ilikuwa ikisikia kwa jirani.

Baada ya mateso ya muda mrefu, msimu huu ukiwa wa 11 kwa timu hiyo kushiriki kimataifa, imefuzu makundi.

Aliyefanya kazi hiyo ni kocha mwenye rekodi nzuri ya michuano ya kimataifa, Florent Ibenge ambaye amewahi kushinda ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na RS Berkane.

Ibenge amefanya kazi kubwa ya kuivusha Azam kucheza makundi kwa mara ya kwanza baada ya wa-tangulizi wake kibao kushindwa akiwemo Boris Bunjak, Joseph Omog, Stewart Hall, George Lwanda-mina na Rachid Taousi.

Ushindi wa jumla wa mabao 9-0 dhidi ya KMKM, umeipa Azam tiketi hiyo baada ya kusubiri kwa muda mrefu. Kumbuka Ibenge huu ni msimu wake wa kwanza klabuni hapo, hajafikisha hata miezi sita tangu atambulishwe.

Tangu kuanzishwa kwa Azam mwaka 2004, imepita takribani miaka 21, klabu hiyo ilikuwa inazishuhudia timu nyingine zikitinga makundi tena zikitumia uwanja wao wa Azam Complex.

Azam iliyoanza kushiriki michuano ya CAF mwaka 2013, ilikuwa haijawahi kucheza makundi ambapo mara mbili imeshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015 na 2024-2025, zote imeishia hatua ya awali.

Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya msimu huu kufuzu makundi, huko nyuma imewahi kujitahidi na kufika hatua ya pili.

Rekodi zinaonyesha katika Kombe la Shirikisho Afrika, Azam mara ya kwanza ilishiriki mwaka 2013 na kuishia hatua ya kwanza, kisha 2014 (hatua ya awali), 2016 (hatua ya pili), 2017 (hatua ya kwanza), 2019–2020 (hatua ya kwanza), 2021–2022 (hatua ya pili), 2022-2023 (hatua ya pili), 2023-2024 (hatua ya kwanza).

Tiketi ya Azam kwenda makundi imekuja chini ya utawala wa Ibenge, akivunja mfupa uliowashinda wa-tangulizi wake.

Azam chini ya Ibenge imecheza mechi nne za mtoano, ikishinda zote kwa kufunga jumla ya mabao 13, ikilinda vizuri nyavu zake kwani hazijatikiswa.

Azam sasa itakuwa inazungumza lugha moja na Simba, Yanga, Namungo na Singida Black Stars, kwani ni timu pekee za Tanzania zilizocheza hatua ya makundi michuano ya CAF, na hata kwenye viwango vya CAF kule itaonekana.

Kabla ya hapo, Simba ndio inaongoza kwa kukusanya pointi nyingi CAF ikiwa nazo 48 ikishika nafasi ya tano Afrika, ikifuatiwa na Yanga (34) ambayo ni ya 12 na Namungo (0.5) ya 77. Singida Black Stars na Azam kwa kuingia makundi, zina uhakika wa kukusanya pointi 0.5, kilichobaki ni kufika mbali zaidi kui-marisha ubora wa nafasi yao CAF.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *