Dar es Salaam. Katika dunia ya sasa, urembo wa mwanamke haupimwi tena kwa vipodozi vya bei ghali au mavazi ya kifahari pekee. Mwanamke wa kisasa amegundua siri kubwa ya urembo wa kudumu ambao ni ule unaotoka ndani.

Ni urembo unaojengwa kupitia lishe bora, mazoezi ya mwili na unywaji wa maji wa kutosha. Huu ndio msingi wa falsafa mpya inayozidi kushika kasi ni mwendo wa kujipenda ni kujitunza.

URE 01

MAANA YA LISHE BORA

Ni mazingira yanayojumuisha chakula na afya kwa wanawake ni muhimu kwa kudumisha ustawi wa jumla, kudhibiti uzito, na kuzuia magonjwa. Mahitaji ya lishe ya wanawake yanaweza kutofautiana kulingana na umri kiwango cha shughuli na hatua ya maisha.

Mtaalamu wa lishe kutoka Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili, Dk Angela Mushi, anasema: “Mwili wa mwanamke una mahitaji maalum ya virutubishi kutokana na mabadiliko ya homoni na majukumu ya kila siku. Ukikosa lishe bora, matokeo yake huanza kuonekana hata kwenye ngozi, nywele na mkao wa mwili.”

Lishe yenye uwiano sahihi wa protini, wanga, mafuta bora, vitamini na madini hufanya kazi ya kimyakimya kuimarisha seli za mwili.

Kwa mfano protini kutoka kwenye samaki, maharage, mayai na karanga hujenga misuli na kusaidia tishu mpya kukua. Hii inamfanya mwanamke kuwa na mwili wenye nguvu, ngozi iliyokaza na nywele zenye afya.

Kwa upande mwingine, vitamini A, C na E kutoka matunda kama parachichi, machungwa na papai hufanya kazi kama kinga dhidi ya uzee wa mapema. Hivyo, lishe bora si tu chanzo cha afya njema, bali pia ni ‘make-up ya asili’ ambayo huangaza bila vipodozi.

URE 02

SIRI YA UREMBO WA ASILI

Maji ni zawadi isiyo na mbadala katika safari ya kujitunza, kila seli mwilini inahitaji maji ili kufanya kazi ipasavyo, ukosefu wa maji mwilini husababisha ngozi kuwa kavu, midomo kupasuka na macho kuonekana yamechoka.

Mtaalamu wa mazoezi na afya, Sophia Nkwabi, anashauri wanawake kunywa angalau glasi nane hadi kumi za maji kwa siku.

“Unapokunywa maji ya kutosha, ngozi yako hujilainisha yenyewe, huna haja ya krimu nyingi maji yanatosha kufanya ngozi yako ionekane yenye uhai na mvuto.

Mbali na maji safi, vinywaji vya asili kama juisi ya mboga (smoothies) au maji ya nazi vinaongeza madini mwilini. Hata hivyo, wanawake wengi hukosea kwa kutumia vinywaji vyenye sukari nyingi kama mbadala wa maji jambo linaloweza kuongeza uzito au kuathiri ngozi,” anasema Sophia.

URE 03

MICHEZO NA MWILI WA MWANAMKE

Daktari Mushi anasema, mazoezi ni rafiki mkubwa wa urembo wa ndani. Wakati mwingine wanawake huona mazoezi kama njia ya kupunguza uzito pekee, lakini ukweli ni kwamba huchangia zaidi kwenye mwonekano wa kiafya na kujiamini.

Mazoezi kama yoga, mazoezi ya nguvu (strength training) na kukimbia huongeza mzunguko wa damu, na hivyo kusaidia ngozi kupata oksijeni ya kutosha. Aidha, mazoezi huchochea mwili kutoa homoni za furaha kama ‘endorphins’ zinazosaidia kupunguza msongo wa mawazo.

“Mwanamke anapofanya mazoezi mara kwa mara, hata mfumo wake wa homoni unakuwa sawa. Hii inasaidia hata katika kudhibiti chunusi na matatizo mengine ya ngozi yanayosababishwa na msongo wa mawazo.

“Kwa wanawake wengi wa mijini, mazoezi yamekuwa sehemu ya mtindo wa maisha iwe ni kutembea asubuhi, kufanya ‘home workouts’ au kushiriki ‘fitness classes’. Hizi si tu shughuli za mwili, bali pia ni njia za kujenga umoja, kujithamini na  kiakili.

UREMBO UNAOTOKA NDANI

Mtaalamu wa lishe, Dk Rehema Mkapa anasema kuwa urembo wa kweli huanza ndani ya mwili, mwanamke anayejitunza hulala vizuri, hula kwa wakati, na kutafuta muda wa utulivu.

“Hakuna krimu inayoweza kuficha uchovu unaosababishwa na lishe duni. Unapokula vizuri, unalala vizuri, na unakunywa maji ya kutosha, hata macho yako yanakuwa na mwanga wa furaha.”

Kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO), wanawake wanaofanya mazoezi na kula lishe bora mara kwa mara hupunguza hatari ya kupata magonjwa sugu kama shinikizo la damu, kisukari na saratani ya matiti.

KUJITUNZA NI KUJIPENDA

Dk Sophia Nkwabi anasema urembo wa mwanamke hautokani na alichovaa, bali mng’ao, afya na furaha kutoka ndani na kwamba anayejitunza huchagua kula chakula chenye faida, kunywa maji ya kutosha, kufanya mazoezi na kujipa muda wa kupumzika.

“Mwanamke mzuri ni yule anayeheshimu mwili wake kwa kuutunza. Lishe bora ni lugha ya upendo kwa nafsi yako, hivyo basi, unapokula chakula bora leo, unalisha zaidi ya tumbo, unalisha mwanga wako wa asili.

“Urembo wa kweli hauwezi kupakwa, bali unaweza kujengwa na mwanamke anayejitunza kwa lishe bora, maji, na mazoezi huangaza kwa urembo usiopimika.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *