Rais wa Marekani Donald Trump amewasili kwenye eneo la kusini-mashariki mwa Asia kwa ziara ya siku tano.

Kwa mujibu wa Pars Today, Rais wa Marekani Donald Trump aliwasili kusini-mashariki mwa Asia siku ya Jumapili kuanza safari yake ya kwanza ya barani Asia tangu aliporudi madarakani huko Marekani. Safari hiyo ya siku tano inajumuisha kuzitembelea nchi za Malaysia, Japan na Korea Kusini na itamalizikia kwenye kushiriki katika mazungumzo yanayotarajiwa sana kati yake na Rais wa China, Xi Jinping. Safari hiyo ya Trump imefanyika huku mvutano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili kubwa zaidi duniani ukifikia kiwango chao cha juu zaidi katika miaka ya hivi karibuni.

Mbali na kuwa kwake safari ya kidiplomasia, ziara ya rais wa Marekani huko kusini-mashariki mwa Asia ni ishara ya kushadidi ushindani wa kimkakati na kiuchumi kati ya Marekani na China. Safari hiyo inaweza kuwa hatua muhimu katika kudhibiti au kuongeza mvutano wa kibiashara, na matokeo yake kwa masoko ya kimataifa na siasa za kikanda yatakuwa muhimu. Kwa mtazamo wa wawekezaji, mazungumzo yaliyopangwa kufanyika wakati wa safari hiyo ya Trump ni ishara ya mabadiliko yanayoweza kutokea katika sera ya ushuru na biashara ya kimataifa, na kwa mtazamo wa viongozi wa kikanda, inachukuliwa kuwa imma ni fursa au tishio kwa ushirikiano wa kiusalama na kiuchumi.

Miongoni mwa malengo ya safari ya Trump barani Asia ni kudhibiti na kupunguza mvutano unaotokana na vita vya ushuru; vita ambavyo vimeanza tena wakati wa urais wa Trump na vimeathiri uchumi wa dunia.

Rais wa Marekani, Donald Trump mwenye uchu wa madaraka, mpenda sifa, mwenye kiu ya kupindukia ya fedha na kiburi

Wakati wa safari hii ambayo Trump ameianzia nchini Malaysia na kukutana na Anwar Ibrahim, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, na kuhudhuria dhifa ya kikazi ya viongozi wa jumuiya ya ASEAN. Lengo la hatua hiyo ni kuwasilisha ujumbe wa nguvu na ushawishi wa Marekani katika eneo hilo kwa kuhudhuria sherehe ya kusaini makubaliano ya amani kati ya Cambodia na Thailand, ambayo Ikulu ya White House inadai Trump alichukua jukumu muhimu kutatua mgogoro wa nchi hizo na kufikiwa makubaliano hayo.

Huko Japan, Rais wa Marekani atakutana na Sanae Takaichi, Waziri Mkuu mpya wa Japan pamoja na Mfalme Naruhito; hatua ambayo si tu itaimarisha uhusiano wa kimkakati wa jadi kati ya nchi hizo mbili, lakini pia inaonyesha kwamba Marekani inajaribu kuleta mlingano sawa wa nguvu katika eneo la Asia-Pasifiki. Kisha huko Korea Kusini, Trump atahutubia mkutano wa viongozi wa biashara wa APEC. Wakati huo huo, mazungumzo yanaendelea ili kukamilisha makubaliano na Korea, Japan na hata China.

Mkutano wa Trump na Xi Jinping ndilo lengo kuu la safari hiyo, ambalo linaweza kuamua mwendo wa uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi China na Marekani. Marekani inahitaji mno mapatano na China kwa maslahi yake ya kiuchumi ndio maana Trump anajaribu kutuma ujumbe wa wazi kwa Beijing kwamba Washington iko tayari kufikia makubaliano, lakini kwa masharti yanayopendekezwa na Marekani. Mbinu hiyo ingawa inaweza kuongeza mvutano kwa muda mfupi, lakini inaunda fursa ya kufafanuliwa upya sheria za masuala ya kiuchumi na mwishowe kufanyika mazungumzo mazito kati ya nchi hizo mbili.

Tunapoiangalia hali ya hivi sasa tunaona wazi kwamba, uhusiano wa Marekani na China ni mgumu zaidi kutengenea ikilinganishwa na huko nyuma. Uchumi wa China unaokuwa kwa kasi ni mshindani mkubwa kwa Marekani, na Washington inajaribu mara kwa mara kuimarisha nafasi yake katika masoko ya Asia na kuendesha vita vikali vya kiuchumi dhidi ya China. Kupitishwa sera kama vile vikwazo vya teknolojia, kupiga marufuku makampuni ya Kichina katika soko la Marekani na vikwazo dhidi ya viwanda muhimu vya China kumefanya mkutano huu wa kidiplomasia kuwa nyeti sana, na matokeo yake yanaweza kuathiri zaidi masuala ya kiuchumi na hadi kwenye sera za kikanda na kimataifa.

Safari hiyo ya Trump pia inaashiria kurejea sera ya kigeni ya Marekani ya kuzingatia uhusiano wa moja kwa moja na wakati huo huo kufanya mazungumzo makubwa kati ya madola makuu ya kiuchumi duniani. Mkutano wa Trump na viongozi wa Japan na Korea Kusini pia unaonesha kuendelea juhudi zake za kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kudhibiti ushawishi wa China. Kwa kuongezea tunaweza kusema kuwa, hatua yoyote mbaya au uamuzi utakaochukuliwa kwa pupa unaweza kuzusha mawimbi mapya ya mivutano katika biashara ya kimataifa na kuhatarisha utulivu wa kikanda.

Sun Chenghao, mtafiti katika Kituo cha Usalama na Mkakati wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Tsinghua cha nchini China anasema hivi  kuhusu jambo hilo: Katika muhula wa kwanza utawala wa wa Trump, mazungumzo ya ngazi za juu kati ya viongozi wa Marekani na China hayakumzuia Trump kuchukua misimamo mikali baadaye kwani ni mtu asiye na mwamana hata kidogo.

Kwa kweli, matokeo ya safari hii, iwe ni makubaliano ya biashara au mwendelezo wa ushindani wa kiuchumi, yanaweza kuunda mwelekeo mpya wa uchumi wa dunia na siasa za kikanda barani Asia kwa ajili ya miaka ijayo. Kwa kweli, safari hii ya Trump barani Asia inaashiria uwanja mpya wa kutanuliana misula ya nguvu za kibiasha na kidiplomasia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *