Dar es Salaam. Mjini YouTube kuna tamthilia moja matata. Ni moja ya tamthilia iliyofanikiwa kuteka nyoyo za Watanzania. Mtaani kila mtu anaizungumzia. Kama siyo wewe, basi mkeo au beki tatu wako.

Sasa mwandaji wa tamthilia hiyo alipata dili la kampuni fulani ya kuonyesha muvi na tamthilia mtandaoni kama ilivyo Netflix.

Na kampuni hiyo ikamtaka kuacha kurusha tamthilia hiyo Youtube ili iwe inaruka kwao pekee. Jamaa akakubali kwa sababu bila shaka dili lilikuwa nono.

Basi akaipeleka tamthilia yake huko kwenye hiyo kampuni na kuwatangazia mashabiki wake kwamba kwa sasa hawataweza kuitazama bure Youtube kama walivyozowea badala yake watakuwa wanailipia Sh3,000 kuitazama kwenye jukwaa hilo jipya.

KISH 01

Unajua majibu ya mashabiki yalikuwaje? Kwanza hawakwenda kuitazama huko kwenye jukwaa jipya la kulipia. Walikwenda wachache sana. Pili, wachache waliokwenda walikuwa wanafanya janjajanja.

Wanaipakua na kuja kuirusha kwenye chaneli zao za Youtube. Na tatu, walianza kutangaza wazi kwamba hawatakwenda kutazama hiyo tamthilia huko kwa sababu zamani walikuwa wanaitazama bure kwanini sasa walipie? Wengine wakasema hawawezi kulipia vitu mara mbilimbili. Walipie bando na bado walipe pesa ili kuitazama. Na wengine mpaka walikuwa wanatamba kwamba wachache waliokwenda huko kutazama wanapakua na kuileta Youtube bure.

KISH 02

Matokeo yake ni kwamba prodyuza aliamua kuirudisha tamthilia yake Youtube baada ya kuona atapoteza watu. Hata hivyo, hata baada ya kuirudisha idadi ya watazamaji wake imepungua ukilinganisha na aliokuwa akiwapata awali.

Kilichomtokea prodyuza ni kitu ambacho nimekuwa nikihubiri kila siku napokutana na watengeneza filamu kwamba jamani acheni tabia ya kuwazowesha Watanzania kutazama kazi za filamu bure kwani wanawazoea kutothamini kazi hizo. Lakini wasanii wamekuwa wagumu kuelewa na kusikiliza huku sababu zao kuu zikiwa mbili.

KISH 03

Kwanza, wanasema eti Youtube inawasaidia kujenga ‘fan base’  kwamba ile idadi ya ‘views na subscribers’ kwenye chaneli zao wanaweza kuitumia kupata dili. Na mimi jibu langu huwa ni kwamba huo upuuzi na kujidanganya.

Mashabiki ambao hawapo tayari kulipa hata senti kumi hawana faida hata ukiwa nao milioni nane. Kwa sababu huwezi kupata pesa moja kwa moja kutoka kwao. Ili kupata pesa inabidi ufanye kazi na watu wanaotaka kutangaza vitu vyao.

Ni namna nzuri ya kujilipa, lakini katu haijawahi kuwa yenye kufaa kwenye usambazaji wa filamu na ndiyo maana hakuna prodyuza mkubwa duniani anayeitumia. Kupata pesa kupitia matangazo huja kama nyongeza. Njia ya kwanza ya kuingiza pesa kupitia kwenye filamu inatakiwa kuwa mauzo ya filamu husika.

KISH 04

Sababu yao ya pili wanasema Youtube inalipa. Ni kweli Youtube inalipa, lakini inabidi utoe sadaka kadhaa ikiwemo kazi zenye ubora hafifu kwa sababu Youtube inataka mambo ya haraka haraka ambayo yanamlazimisha mwandaaji kufanya kazi mbiombio bila weledi ilimradi iende mtandaoni kabla watazamaji hawamjasahau na kuhamia kwa mtu mwingine.

Pia licha ya kwamba Youtube ina pesa, ila pesa yake ni kidogo kulinganisha na ile ambayo wasanii wa filamu wanatakiwa kupata. Na ndiyo maana wasanii wa filamu wa Youtube wengi hawasimami kiuchumi. Wanakuwa wanapata pesa ya ‘kuwa hai’, lakini ukweli ni kwamba msanii anatakiwa kupata zaidi ya hiyo.

Rai yangu nilishaisema hapo juu na naendelea kuirudia tuache kuwazoesha Watanzania kutazama kazi za sanaa bure. Inawadumaza, inashusha thamani ya kazi za sanaa na matokeo ni kwamba wasanii watabaki kuwa masikini siku zote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *