
Tanzania sasa ina furaha baada ya Klabu zake zote nne kutinga hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika baada yakufanya vizuri katika raundi ya pili ya mashindano hayo.
Klabu hizo nne ni Simba na Yanga ambazo zimeingia katika hatua ya makundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Singida Black Stars na Azam FC ambazo zimetinga katika hatua hiyo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika kuna uwezekano wa Yanga na Simba kupangwa au kutopangwa kundi moja kutegemeana na vyungu ambavyo kila moja itawekwa katika droo ya hatua hiyo itakayochezeshwa Novemba 3, 2025 huko Afrika Kusini.
Hata hivyo kukutana au kutokutana kwa Yanga na Simba katika hatua ya makundi kutategemea zaidi matokeo ya mchezo wa marudiano wa raundi ya pili ya mashindano hayo baina ya RS Berkane ya Morocco na Al Ahli Tripoli ya Libya.
Mchezo wa kwanza baina ya timu hizo uliochezwa Libya jana, Tripoli na Berkane zilitoka sare ya bao 1-1.
Kama Berkane itasonga mbele na kuingia hatua ya makundi, hakutakuwa na uwezekano wa Simba na Yanga kupangwa kundi moja katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Ikiwa Berkane itatolewa na Al Ahli Tripoli, Yanga na Simba hazitoweza kukutana kwenye hatua hiyo ya makundi.
Berkane ikisonga mbele, maana yake itawekwa katika chungu cha kwanza katika uchezeshaji wa droo pamoja na timu za Al Ahly, Mamelodi Sundowns na Esperance huku Simba na Yanga zikiwa katika chungu cha pili hivyo kwa mujibu wa utaratibu wa upangaji makundi, timu zilizo katika chungu kimoja haziwezi kupangwa katika kundi moja.
Iwapo RS Berkane itatolewa, maana yake Simba itawekwa katika chungu cha kwanza na hivyo inaweza kukutana na Yanga ambayo itakuwa katika chungu cha pili.
Ukiondoa Simba na Yanga, timu za nchi nyingine ambazo zinaweza kukutana katika makundi ni RS Berkane na FAR Rabat zote za Morocco na MC Alger na JS Kabylie za Algeria.