
Mapigano yalipamba moto jana Jumapili katika mji uliozingirwa wa al Fasher huko Sudan katika jimbo la Darfur Kaskazini, huku kundi la wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) likidai kuiteka kambi ya jeshi la Sudan (SAF).
Msemaji wa wanamgambo wa RSF amesema kwamba wapiganaji wa kundi hilo wamefanikiwa kutwaa kambi hiyo ya jeshi kwa kuvunja mgongo wa jeshi la Sudan na washirika wake na kuidhibiti kikamilifu.
Msemaji wa RFS ameyataja mafanikio hayo kuwa hatua muhimu ya mabadiliko, na kwamba ni hatua ya kuelekea kwenye ujenzi wa taifa jipya ambalo Wasudani wote watashiriki katika kulianzisha kulingana na matarajio yao ya uhuru, amani na haki.”
Video iliyorushwa katika mitandao ya kijamii na RSF inawaonyesha wapiganaji hao wakisherehekea mbele ya kambi hiyo ya kijeshi. Wanamgambo wa RSF wameidhibiti kambi hiyo ya jeshi la Sudan baada ya siku kadhaa za mapigano makali.
Inafaa kuashiria hapa kuwa wanamgambo wa RSF walikuwa wameuzingira mji wa al Fasher kwa miezi 18 sasa hwakipambana na jeshi la Sudan.
Duru za kijeshi aidha zimeeleza kuwa licha ya wanamgambo wa RSF kutwaa kambi hiyo ya jeshi la Sudan, lakini hakukuwa na mwanajeshi yoyote wakati wa oparesheni hiyo.