
Mbeya. Jeshi la Zimamoto na uokoaji Mkoa wa Mbeya limesema matukio ya majanga na ajali za moto zilizokuwa zimeshamiri mkoani humo huenda zikabaki historia baada ya kupokea magari tisa ya kisasa kukabiliana na matukio hayo.
Akizungumza leo Oktoba 27, 2025 wakati wa kupokea magari hayo, Kaimu Kamanda wa Jeshi hilo mkoani humo, Gervas Fungamali amesema awali walikuwa wakipata changamoto kukabiliana na matukio hayo kutokaba na upungufu wa vifaa.
Amesema Jeshi hilo lilikuwa na magari mawili, hivyo upatikanaji wa magari tisa na ya kisasa yanaenda kusaidia ufanisi wao katika kukabiliana na majanga ya moto na ajali za barabarani.
“Niwahakikishie wananchi mkoani Mbeya kwamba usalama wao na mali zao viko salama, tutatumia vyema vifaa hivi kutimiza wajibu wetu na tutavitunza vizuri tuweze kufikia malengo, zaidi tunaishukuru Serikali,” amesema Fungamali.
Kamanda huyo ameongeza kuwa kwa wiki hupokea matukio matatu ya ajali za moto huku akiwaomba wananchi kutochoma hovyo moto haswa kipindi hiki cha kiangazi akiahidi jeshi hilo kuendelea kutoa elimu katika mikusanyiko ya watu.
Akizindua magari hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa ameliomba jeshi hilo kutunza magari hayo na kuwafikia wananchi kwa elimu namna ya kujikinga na majanga ya moto.
“Hakuna sababu kujua gharama ya magari haya, kwa sababu hata kwa macho unagundua ni fedha nyingi sana, sasa niwaombe msikae ofisini, nendeni kwa wananchi muwape elimu na tunzeni vyema magari haya,”amesema Malisa.
Mmoja wa wananchi walioshuhudia mapokezi ya magari hayo, Benson Muya amesema vifaa hivyo huenda ikawa sehemu ya kuwafikia wananchi wengi wanaokumbwa na majanga ya moto.