Watu 12, wakiwemo watalii, wanahofiwa kufariki dunia katika ajali ya ndege iliyotokea katika eneo la Vyungwani, Matuga, Kaunti ya Kwale, mapema leo Jumanne.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini Kenya (KCAA), Emile Arao, amethibitisha tukio hilo akisema ndege hiyo yenye usajili 5Y-CCA ilikuwa ikielekea Uwanja wa Ndege wa Diani.

Ajali hiyo imetokea mapema Jumanne wakati ndege hiyo ndogo ilipokuwa ikielekea kwenye Hifadhi ya Kitaifa ya Maasai Mara.

Ajali hiyo imetokea katika eneo lenye vilima na misitu, takriban kilomita 40 (maili 25) kutoka uwanja wa ndege wa Diani.

Awali Kamishna wa Kaunti ya Kwale, Stephen Orinde aliiambia The Associated Press kwamba shughuli za uokoaji zilikuwa zikiendelea mapema leo katika eneo hilo.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kenya hapo awali ilisema kwamba watu 12 walikuwa ndani ya ndege hiyo, lakini ripoti ya awali ilisema kulikuwa na abiria 10 ndani yake, wakijumuisha Wahungari wanane na Wajerumani wawili.

Taarifa iliyotolewa na shirika la ndege la Kenya Mombasa Air Safari imesema: “Kwa masikitiko, hakuna manusura (…) Tunasikitika sana kuripoti kwamba, kwa mujibu wa taarifa za awali, kulikuwa na abiria 10, wakiwemo Wahungari 8, Wajerumani 2 na mfanyakazi mmoja wa Kenya (Kapteni) ndani ya ndege”.

Mamlaka bado hazijabaini chanzo cha ajali hiyo. Kaunti ya Kwale imekuwa ikishuhudia mvua kubwa tangu saa tisa usiku wa kuamkia leo.

Maasai Mara ni kivutio maarufu cha watalii, kinachojulikana kwa uhamaji wa kila mwaka wa nyumbu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *