Dar es Salaam. Uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China umechukua sura mpya, baada ya kugeuka lango la soko la kimataifa kati ya mataifa haya mawili.
Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema maonyesho ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa (CIIE), yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza biashara na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na China.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwaaga wafanyabiashara wa Kitanzania wanaokwenda kushiriki maonesho hayo, jana Jumatatu Oktoba 27, 2025, Balozi Mingjian amesema maonyesho ya mwaka 2024 yalihudhuriwa na mataifa 252, yakionyesha bidhaa mbalimbali zikiwemo za kilimo na viwanda.
“Mataifa 252 yalishiriki maonyesho ya mwaka 2024 ambapo bidhaa mbalimbali zikiwemo za kilimo na dawa zilioneshwa,” amesema Balozi Mingjian.
Amebainisha maonyesho hayo ni sehemu ya maono ya Rais wa China, Xi Jinping ya kuifanya nchi hiyo kuwa kitovu cha biashara za kimataifa, akisema CIIE imekuwa mlango wa Tanzania katika kuwezesha mabadilishano ya bidhaa na ukuaji wa uchumi duniani.
“CIIE imekuwa mlango muhimu kwa Tanzania katika mabadilishano ya bidhaa kimataifa na kukuza uchumi wa dunia,” amesema Mingjian.
Ameongeza maonyesho ya mwaka huu yatakayofanyika jijini Shanghai yatakutanisha mamia ya mataifa ambapo wadau watafanya biashara.
Balozi Mingjian aliipongeza Tanzania kwa kuwa mgeni rasmi mwaka 2024 katika maonyesho ya sita ambayo Watanzania waliendelea kushiriki jijini Shanghai.
“Tanzania kupitia bidhaa za mazao ya kilimo imeweza kufungua milango ya mahusiano ya kibiashara baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na wale wa China,” amesema Mingjian.
Amesema Rais wa China, Xi Jinping, anaendelea kuifanya China kuwa kitovu cha biashara za kimataifa, na kutokana na uhusiano mzuri kati yake na Rais Samia Suluhu Hassan, Tanzania imekuwa mdau muhimu katika maonesho hayo.
“Uhusiano mzuri wa viongozi wetu umepelekea ukuaji wa uchumi na mwingiliano wa kibiashara baina ya mataifa haya, hatua ambayo baadhi ya mataifa ya magharibi yanaiona kama tishio la ushindani wa kiuchumi,” amesema Mingjian.
Akiwakaribisha Watanzania kuchangamkia maonyesho hayo, amesema China inahitaji zaidi bidhaa kutoka Tanzania, huku Tanzania ikihitaji bidhaa kutoka China, jambo linalojenga uhusiano wa kudumu wa kiuchumi.
“Zikiwa zimesalia siku tisa kabla ya maonesho kuanza, nawatakia kila la heri washiriki wote kwa faida ya biashara zenu na mataifa yenu kwa ujumla.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa Tanzania (Tantrade), Latifa Hamis, amesema ni jambo la kujivunia kuona uhusiano wa Tanzania na China ukiunda jukwaa muhimu la kunadi na kuongeza fursa za masoko kwa bidhaa za Tanzania.
“Ushiriki wa Watanzania katika maonesho yaliyopita huko Shanghai ulituwezesha kupata mafanikio makubwa ambapo Tanzania imenufaika na mikataba mbalimbali iliyosainiwa kupitia maonesho hayo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 17, hatua iliyoongeza fursa za biashara na masoko mapya,” amesema Hamis.
Amewataka washiriki wa mwaka huu kuwa wabunifu na kufichua fursa mpya wanazokutana nazo nchini China.
“Tunawahimiza washiriki kuwa na jicho la kutambua fursa mpya ambazo zinaweza kuwaongezea tija katika biashara zao. Bidhaa za Tanzania zina ubora wa kimataifa, hivyo waendelee kuwaunga mkono wazalishaji wa ndani,” amesema Hamis.
Balozi wa China nchini Tanzania, Mingjian akiwa na Mkurugenzi wa maonesho ya kimataifa ya biashara nchini, Latifa Hamis katika warsha ya kuwaaga wafanyabiashara wa Tanzania jijini Dar es Salaam, kwenda kushiriki maonesho ya CIIE jijini Shanghai nchini China.
Miongoni mwa washiriki, Emmanuel Mabula, Ofisa Masoko wa Zuchu Wine kutoka Dodoma, amesema Wachina wamesaidia kinywaji hicho kujulikana na kufungua masoko ya kimataifa.
“Kupitia maonesho yanayofanyika China, tumefanikiwa kukuza uzalishaji na kuzalisha ajira nyingi katika kampuni yetu,” amesema Mabula.
Naye Jackson Mponela, Mkurugenzi wa kampuni ya CDTF – Enterprises Company Limited inayojihusisha na uzalishaji wa asali, amesema kushiriki maonyesho ya kimataifa nchini China kumewezesha kampuni yao kupata faida kubwa na kukuza shughuli za kiuchumi.
“CIIE imetuwezesha kupata faida kubwa, kukuza kampuni yetu na kuchangia katika uchumi wa Taifa kwa ujumla,” amesema Mponela.
Kwa upande wake, Meneja wa Maonyesho ya CIIE nchini China, Wang Xiangyu, amesema banda la Tanzania mwaka huu litakuwa na ukubwa wa mita za mraba 22 na litakuwa na bidhaa mbalimbali zikiwemo mwani wa Zanzibar, sanaa za Tingatinga, kahawa, parachichi, mvinyo na mazao mengine ya kilimo na viwanda.
“Tanzania ni moja ya mataifa yanayonufaika pakubwa na ushiriki wake katika maonesho ya CIIE, itaendelea na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na China,” amesema Wang.
Amesema jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kujenga mahusiano mema na China zimewezesha Taifa hilo kuwekeza zaidi katika biashara nchini Tanzania.
“Kwa jitihada za Rais Samia, China itaendelea kuwa mshirika muhimu wa biashara na uwekezaji na kushiriki maonesho ya Sabasaba nchini Tanzania,” amesema Wang.
Maonesho ya nane ya CIIE yanatarajiwa kufanyika Novemba 5 hadi 10, 2025 jijini Shanghai, yakishirikisha zaidi ya mataifa 180 kutoka duniani kote.