Dar es Salaam. Fasheni zinakuja na kupotea, ila hii ya miwani za msanii wa Bongo Movie na aliyewahi kushiriki shindano la Miss Tanzania, Irene Uwoya ndiyo habari ya mjini.
Ni hivi. Uwoya amekuwa akiweka picha za mionekano tofauti akiwa na miwani za aina na staili mbalimbali na kuzua gumzo katika mitandao ya kijamii, mwenyewe hajasita kutolea ufafanuzi wa kile anachokiposti kuhusu miwani hizo za aina yake.
Mrembo huyo anasema anachokifanya wengi hawajui ila yeye ni mwanamitindo.
“Mimi mbali na kuigiza ni mwanamitindo pia, hivyo nimeona kuja na kitu tofauti kitakachoweka alama kwenye ubunifu na urembo na kuniweka kwenye utambulisho mpya.
“Ndiyo maana nikabuni fasheni ya aina ya miwani zenye fremu kubwa na zenye mwanga makali. Yaani ziko tofauti tofauti na kwa sasa zimekuwa ndiyo habari ya mjini. Watu wengi wamekuwa na shauku ya kutaka kuzivaa na si unaona nimeanzisha wadada wengi wamefuata na siku zinavyozidi kwenda zitavaliwa sana na wenye maduka wengi wataona ni dili.”
Anasema miwani zake huwa anaagiza Marekani na hapa anataja na bei zake;
“Nina miwani nyingi sana, yaani hapa bado sana kumaliza kuzivaa, nimechukua aina tofauti tofauti na simalizi kuvaa leo wala kesho, huwa namwagiza mtu kutoka Marekani na hazina pesa nyingi ni kuanzia Dola 22 sawa na Sh55,000.”
Watu wengi hasa mitandaoni wamekuwa wakihoji kuhusu mavazi anayovaa na kujiposti Instagram yakiwa yanamwonyesha sehemu kubwa ya mwili wake, licha ya awali kudai ameokoka na hapa anawaweka wazi;
“Jamani jamani jamani, sawa nimeokoka ila kwenye mavazi siwezi kubadilika kwani kinachoniongoza mimi ni imani yangu na siyo mihemko ya watu. Embu watu waache. Kufanya wokovu ni mgumu sana na uzuri mimi siigizi nimeokoa, kwa wanaonifatilia nafanya sana kazi za utumishi wa Mungu hii ni kubwa sana kuliko watu wanavyonifikiria.”
Uwoya anasema yote hayo anayasikia ikiwamo kuwa na stress za mapenzi, lakini ambacho wengi hawajui ni sasa hivi ameipisha kidogo mitandao ya kijamii ili watu waendelee na shughuli zao kwani yanampotezea muda mwingi na kufeli malengo yake.
“Kwa sasa nimeipisha mitandao maana kila kukicha ilikuwa ni mimi kisa tu kutangaza nimeokoa. Hata hivyo, mwishowe nilikubali tu kila kitu, nikakaa kimya na walisema na wakamaliza yote, wakatulia tuli.”
VIPI KUHUSU KUIGIZA
“Mimi sijaacha kuigiza pamoja na kuokoka kwangu, yaani kitendo cha mtu kuokoka hakiwezi kumzuia mtu kufanya mambo mazuri ambayo aliyokuwa anayafanya na watu wakafurahi kabla ya kuokoka.”
KUNA KAZI INAKUJA
Kumekuwa na maswali mengi kwa mashabiki wake juu ya ukimya wake hasa kwenye kazi na baada ya kuokoka wengi wakaona ndiyo mwisho wa kufanya filamu, lakini mwenyewe anasema bado yupo kwenye fani na watu watarajie kazi mpya itakayowabamba.
“Niliona ‘comment’ za mashabiki wangu wengi wakilalamika na kuingia simanzi katika safari yangu hii ya wokovu basi nitaacha kuigiza. Sasa nimewaondoa hofu kwa kuwaletea Tamthilia itakayoitwa ‘Upepo ‘ itakayoanza Novemba 8, 2025 kwenye channel ya DSTV,” anasema na kuongeza katika tamthilia hiyo amecheza nafasi tofauti ya mke mwema mwenye siri nzito na mavazi ya kitumishi kama anavyojiita sasa.
MAISHA YAMEBADILIKA, AIKUMBUKA 2024
Anasema hatosahau mwaka 2024 kwani ulibadili kwa kiasi kikubwa maisha yake baada ya kuokoka na hataki kabisa kurudi katika matatizo hasa mwaka huu 2025.
“Kitu napenda ni kuokoka na kuwa mtumishi wa Mungu na kuweka kumbukumbu ya mwaka 2024, nilibadili maisha yangu na kuanza safari ya utumishi. Sikutaka mwaka huu 2025 kuingia na matatizo ya miaka ya nyuma kabla sijaokoka.”