BAADA ya kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mashujaa, kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda amesema anaamini kikosi chake kitafanya vizuri dhidi ya Azam kwenye mechi itakayochezwa Novemba 5, mwaka huu huku akiweka wazi kuwa wametibu tatizo lililokuwa likiwasumbua, hivyo hawatarudia makosa.

Mechi hiyo imepangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa kuanzia saa 1:00 usiku.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mgunda ameweka wazi kuwa, anamini ataenda kuifunga Azam kutokana na maboresho ya kikosi chake ambacho sasa kimeimarika.

Amesema anatambua Azam ni timu nzuri, ina morali kubwa baada ya kutoka kuandika rekodi ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza, sambamba na wachezaji wazuri.

MGU 01

Kwa kulitambua hilo, Mgunda amesema akiwa kocha amewajenga vijana wake vyema kisaikolojia ili kuhakikisha wanashinda mechi hiyo kufikia malengo waliyojiwekea.

Mgunda amesema ugumu wa ligi unamfanya yeye kama kiongozi wa benchi la ufundi kutumia mbinu zote ili kuisaidia timu hiyo kufikia malengo huku akiweka wazi kwamba hakuna timu rahisi, zote zinatoa ushindani, hivyo hawana hofu kukabiliana nazo. “Maandalizi kisaikolojia na kimbinu yameenda vizuri, naamini wachezaji wangu watafanyia kazi kila kitu nitakachowaelekeza kwa lengo la kuhakikisha tunatumia vyema uwanja wa nyumbani kupata matokeo ya ushindi,” amesema Mgunda.

Amesema kuna muda mzuri wa kujiweka kwenye ushindani licha ya timu kupata mapumziko ya mara kwa mara kutokana na namna ratiba ilivyopangwa.

MGU 02

Namungo imecheza mechi tano za Ligi Kuu Bara msimu huu na kukusanya pointi tano baada ya kupokea vipigo viwili, sare mbili na kushinda moja.

Timu hiyo ilianza na sare ya bao 1-1 dhidi ya Pamba Jiji, ikaichapa Tanzania Prisons bao 1-0, kisha ikapigwa 3-0 na Simba, ikafuatia sare ya 1-1 dhidi ya JKT Tanzania, ikaenda kufungwa 1-0 na Mashujaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *