ALICHOKIFANYA Prince Dube katika mechi dhidi ya Silver Strikers ambayo Yanga ilishinda 2-0 na kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu Jumamosi iliyopita Oktoba 25, 2025, kimewaacha wengi na maswali, lakini kocha wake ametaja kinachomsumbua.

Mzimbabwe huyo aliyeanzishwa kuongoza safu ya ushambuliaji katika mechi hiyo ya uamuzi ambayo Yanga ilitakiwa ishinde kwa angalau mabao 2-0 ili ifuzu makundi baada ya ugenini kufungwa bao 1-0, alitolewa dakika ya 80 huku akikosa zaidi ya nafasi tano, akaingia Andy Boyeli.

Wakati Dube akishindwa kufunga, Yanga ilipata mabao kupitia beki Dickson Job dakika ya sita na kiungo Pacome Zouzoua dakika ya 32 hali iliyowafanya wavuke.

ZENG 01

Dube ambaye alijiunga na Yanga akitokea Azam msimu uliopita amekuwa na wakati mgumu Yanga msimu huu, baada ya uliopita kufanya vizuri akiisaidia timu hiyo kutwaa makombe yote ya ndani, Ngao ya Jamii, Kombe la Muungano, Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, huku akifunga mabao 13 katika Ligi Kuu Bara, moja nyuma ya Clement Mzize, pia akizidiwa matatu na kinara wa jumla, Jean Charles Ahoua wa Simba.

Si Dube pekee, hata Andy Boyeli hana wakati mzuri ikiwa ni msimu wake wa kwanza Yanga akitua kikosini hapo akitokea Sekhukhune ya Afrika Kusini.

Washambuliaji hao wote msimu huu wamepewa muda wa kucheza Yanga wakipishana, ukiona ameanza Dube, basi Boyeli anaingia baadaye, lakini wote hawana makali. Siku nyingine anaanza Boyeli, Dube anafuatia.

ZENG 02

Hata hivyo, ni Dube pekee amecheka na nyavu mara moja katika mechi nane za mashindano ilizocheza Yanga msimu huu, ambapo moja Ngao ya Jamii, tatu Ligi Kuu Bara na nne Ligi ya Mabingwa Afrika.

Dube amefunga bao moja katika mechi hizo dhidi ya Wiliete wakati Yanga ikishinda 3-0 ugenini hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Kwenye ligi na Ngao ya Jamii, hajafunga.
Katika ishu ya ukame wa mabao, Boyeli hazungumzwi sana, lakini Dube amekuwa midomoni mwa wengi baada ya kushindwa kuzitumia vizuri nafasi nyingi anazopata.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Patrick Mabedi akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 27, 2025, amesema: “Dube amefanya mambo mengi mazuri. Nafahamu ana mzigo mkubwa mabegani mwake. Kwa uwezo alionao atakaa sawa. Kuna presha nyuma yake lakini hiyo ni kawaida kwa wachezaji wakubwa popote pale. Usipofunga lazima maswali yawe mengi. Ni suala la muda Dube atarejea kwenye makali yake, sina wasiwasi.”

ZENG 03

Dube ambaye aliyetumikia Azam FC kwa misimu mitatu na nusu, kisha akahamia Yanga, amekuwa hana namba nzuri katika kucheka na nyavu. Ndani ya Azam, katika mechi 54 za Ligi Kuu Bara alifanikiwa kufunga mabao 34.

Msimu uliopita ambao ulikuwa wa kwanza kwake ndani ya Yanga, alifunga mabao 13 katika Ligi Kuu Bara akicheza mechi 27 kwa dakika 1,829, alifanikiwa kutoa asisti nane.

ZENG 04

Wakati washambuliaji wa Yanga wakiwa kwenye wakati mgumu, Pacome amekuwa akifanya kazi kubwa ya kufunga kwani katika mechi hizo nane za msimu huu kwenye mashindano yote wakati Yanga ikifunga mabao 13, kiungo huyo kutoka Ivory Coast ametikisa nyavu mara tatu. Anayefuatia ni kiungo Aziz Andabwile akifunga mabao mawili. Wengine waliofunga bao mojamoja ni beki Dickson Job, Edmund John (winga), Mudathir Yahya (kiungo), Lassine Kouma (kiungo), Maxi Mpia Nzengeli (winga), Mohamed Hussein (beki), Celestine Ecua (winga). Pia Dube naye ana moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *