Wimbi jipya la uungaji mkono kwa Wapalestina barani Afrika limekwenda sambamba na kulaani vitendo vya kijinai vya utawala haramu wa Israel.
Raia wa Tunisia walikusanyika mjini Tunis, mji mkuu wa Tunisia, Jumamosi jioni, Oktoba 25, kuwaunga mkono mateka wa Kipalestina walioachiliwa huru kutoka mikononi mwa Israel baada ya kutekelezwa kwa usitishaji vita huko Gaza, na kulaani kitendo cha Israel cha kuwadhalilisha wafungwa wa Kipalestina. Mkusanyiko huo ulifanyika kwa mwaliko wa shirika lisilo la kiserikali la “wasaidizi wa Palestina” chini ya kichwa “kutoka jela mpaka kuchomoza jua la mateka wetu…utukufu wenu ndio utukufu wetu.”
“Riyadh Zahafi,” msemaji wa shirika lisilo la kiserikali la wasaidizi wa Palestina alisema: “Suala la wafungwa ni moja ya haki za kimsingi za Wapalestina, kwani zaidi ya Wapalestina 10,000 walishikiliwa katika jela za Kizayuni.”
Amesema: “Mbali na kila aina ya adhabu za kinyama, wafungwa na mateka wa Kipalestina wanapata mateso na unyanyasaji wa kila namna. Vitendo hivyo vinafichua sura halisi ya utawala wa Kizayuni; utawala ambao umefanya mauaji ya kimbari na mateso ya kila namna.”
Hivi majuzi, zilisambaa picha za video zikiwaonyesha maafisa wa usalama wa Israel wakiwatesa na kuwadhalilisha wafungwa wa Kipalestina katika jela ya Katzput iliyoko Negev (Palestina inayokaliwa kwa mabavu kusini).
Pia, picha zilizochapishwa na tovuti ya Kiebrania zilionyesha kuwa wafungwa wa Kipalestina wanaishi katika mazingira magumu na wanafanyiwa upekuzi kwa mbinu kali. Kufuatia kutekelezwa kwa usitishaji vita huko Gaza, Wapalestina 1968 waliachiliwa kutoka magereza ya Israel, 250 kati yao walihukumiwa kifungo cha maisha.
Katika hatua nyingine ya kuwaunga mkono Wapalestina, raia wa Morocco walifanya maandamano dhidi ya Wazayuni kulaani kuendelea mashambulizi ya wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza. Ijumaa jioni, Oktoba 24, raia wa Rabat waliingia barabarani na kupiga nara dhidi ya Wazayuni kulaani kuendelea kwa mashambulizi ya wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Raia wa Morocco walikusanyika mbele ya bunge la nchi hiyo na kupaza sauti wakisema: “Tunapinga uvamizi huo.” Walishikilia mabango, baadhi yao yakisomeka: “Palestina lazima iwe huru” na “muqawama hadi ukombozi wa Palestina.” Maandamano hayo yalifanyika kwa mwaliko wa shirika lisilo la kiserikali la “Action for Palestine,” na washiriki walilaani kuendelea kukiuka usitishaji vita huko Gaza kunakofanywa na jeshi la Israel.
Hivi karibuni utawala wa Israel na harakati ya Hamas walitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano, yaliyopatanishwa na Marekani, ambapo jeshi la Israel litaondoka Gaza, zoezi la ubadilishanaji wafungwa litafanywa kati ya pande hizo mbili, na misaada ya kibinadamu itatumwa Gaza.
Hii ni pamoja na kuwa, kwa mujibu wa ripoti, tangu kuanza kutekelezwa usitishaji vita katika ukanda huu, utawala wa Israel umekiuka usitishaji vita huo zaidi ya mara 80 na kusababisha kuuawa shahidi Wapalestina 97.
Harakati za wananchi katika nchi hizi mbili za Kaskazini mwa Afrika za kuunga mkono kadhia ya Palestina zinaakisi utendaji ulio dhidi ya Uzayuni katika bara la Afrika. Kwa ujumla, mtazamo wa watu wa Afrika, hasa katika nchi za Kiislamu za kaskazini mwa bara hilo, kuhusiana na Israel, ni mchanganyiko wa mshikamano wa kihistoria na Palestina, uzoefu wa ukoloni, na athari za kijiografia za kisasa.
Mtazamo huu unaweza kufupishwa katika nukta kadhaa kuu:
Mshikamano wa kihistoria na Palestina

– Nchi nyingi za Kiafrika, hasa zile ambazo zimepitia tajiriba ya ukoloni na mapambano ya kudai uhuru, zinajihesabu kuwa zina hatima ya pamoja na watu wa Palestina.
– Viongozi wa ukombozi wa Afrika kama vile Nelson Mandela wameunga mkono mara chungu nzima harakati za Palestina na kulinganisha uvamizi wa Israel na utawala wa makaburu wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Misimamo ya nchi za Kiislamu za Kiafrika
– Nchi za Kiislamu kama vile Sudan, Mali, Mauritania na Algeria kawaida huwa na misimamo mikali zaidi dhidi ya Israel na hutetea haki za Wapalestina.
– Hata hivyo, baadhi ya nchi kama vile Morocco na Sudan, zimeanzisha uhusiano wa kawaida na Israel katika miaka ya hivi karibuni, chini ya mashinikizo ya kidiplomasia na kiuchumi, hatua ambayo imekabiliwa na maoni hasi ya umma katika nchi hizo.
Maoni ya umma na vyombo vya habari
– Katika jamii nyingi za Kiafrika, hususan kati ya Waislamu, Israel inatambuliwa kuwa nembo ya ukandamizaji na uvamizi.
– Vyombo vya habari vya ndani na mitandao ya kijamii katika nchi za Kiafrika mara nyingi huangazia habari kuhusu mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza na Yemen kwa sauti ya kukosoa, na huruma kwa wahanga wa Palestina ni jambo la kawaida.
Pengo kati ya misimamo rasmi ya serikali na ya wananchi
– Katika hali ambayo, baadhi ya serikali za Kiafrika zimepanua uhusiano wao na Israeli kwa sababu za kiuchumi au kisiasa, maoni ya umma katika nchi nyingi za bara hilo yanaendelea kukosoa Israel.
– Pengo hili limesababisha baadhi ya serikali kuchukua misimamo ya tahadhari zaidi katika majukwaa ya kimataifa ili kuepusha radiamali za ndani.