London, England. Baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Crystal Palace katika mchezo uliopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Emirates, ushindi uliowafanya vijana wa Mikel Arteta kuendelea kukaa kileleni mwa Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi nne.
Lakini pamoja na ushindi huo, kocha Mikel Arteta ana sababu ya kuwa na wasiwasi baada ya wachezaji wake wanne kuumia katika mchezo huo.
Nyota wa England Declan Rice, beki William Saliba, na mlinzi Riccardo Calafiori wote walilazimika kutolewa uwanjani kutokana na majeraha, huku Gabriel Martinelli naye akiwa na hali ya kutia wasiwasi.
Akizungumza baada ya mechi, Arteta alisema hajui muda kamili ambao Rice atakuwa nje ya uwanja.
“Kwa Declan kwa kweli sijui. Ilionekana kama amepigwa, labda ni misuli ya ndani. Tutafanyia vipimo kujua zaidi,” alisema kocha huyo.
Saliba ndiye alikuwa wa kwanza kutoka baada ya kipindi cha kwanza, nafasi yake ikichukuliwa na Cristhian Mosquera. Baadaye Rice alipata maumivu dakika kumi kabla ya mchezo kumalizika na nafasi yake kuchukuliwa na Mikel Merino, huku Calafiori naye akitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Piero Hincapié aliyekuwa akicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu.
Arteta pia alithibitisha kuwa Martinelli atapimwa na madaktari baada ya kusema alihisi kitu kwenye mguu wake, huku akiongeza kuwa nyota mwingine Bukayo Saka alitolewa kwa tahadhari kwa sababu alikuwa anatoka kwenye ugonjwa.
“Saka alikuwa mgonjwa, hakufanya mazoezi vizuri. Tulikuwa hatujui kama ataweza kucheza,” aliongeza Arteta.
Arsenal tayari inawakosa nahodha Martin Ødegaard, ambaye atarejea baada ya mapumziko ya kimataifa ya mwezi Novemba, pamoja na Noni Madueke, Kai Havertz na Gabriel Jesus ambao wote bado wanauguza majeraha.
Baada ya mechi hiyo, Arsenal inajiandaa kuvaana na Brighton katika raundi ya nne ya Kombe la Carabao Jumatano Oktoba 29, 2025 kabla ya safari ya kwenda kukutana na Burnley wikendi ijayo, kisha kucheza mechi ya katikati ya wiki kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Slavia Prague na baadaye kumalizia na Sunderland kabla ya mapumziko ya kimataifa.