Akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva Uswisi hii leo, Necephor Mghendi, Afisa kutoka shirikisho la Msalaba Mwekundu na Hilal Nyekundu, (IFRC) amesema,
“Takribani watu milioni moja wako hatarini, zikiwemo familia ambazo bado zina madhara ya Kimbunga Beryl. Kumbuka, ni miezi 16 tu imepita. Kimbunga Melissa kinasonga kwa kasi ndogo sana, lakini pia kina uwezo mkubwa wa kuleta mvua nyingi kupita kiasi, mawimbi makubwa ya baharini, na upepo mkali unaoweza kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu, kutenga jamii na kukatiza huduma muhimu kwa siku kadhaa, labda hata wiki. Tishio la kibinadamu ni kubwa na la haraka.”
Ameongeza kuwa kuwa kimbunga hicho cha kiwango cha daraja la tano “kitakuwa chenye nguvu zaidi duniani mwaka huu, kikiweka maisha ya watu milioni moja hatarini, ikiwemo familia ambazo bado zinajikongoja kutokana na madhara ya Kimbunga Beryl kilichoikumba Jamaika miezi 16 tu iliyopita.”
Mwonekano wa angani wa nyumba zilizoharibiwa na Kimbunga Beryl huko Jamaika, ambacho kiliacha uharibifu mkubwa katika parokia za kusini za Clarendon, Manchester, na St. Elizabeth.
Majengo yataharibika, maji yatafurika
“Paa za nyumba zitaezuliwa. Maji ya mafuriko yataongezeka. Upweke utakuwa hali halisi kwa wengi,” amesema Necephor Mghendi
Anne-Claire Fontan, mtaalamu wa vimbunga kutoka Shirika la Hali ya Hewa Duniani la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani (WMO), kwa upande wake ameonya kwamba “uharibifu kwa kina wa miundombinu unatarajiwa,” akirejelea kauli ya Kituo cha Kitaifa cha Vimbunga cha Marekani kilichoko Miami.
Ameongeza kuwa “Sijawahi kuona sentensi kama hii kabla, athari kubwa inatarajiwa Jamaica.”
Upepo mkali, mvua kubwa na mafuriko
Kimbunga Melissa kinaripotiwa kuwa na kasi ya upepo wa kilomita 280 kwa saa, kikiendelea kuelekea magharibi mwa Jamaica asubuhi ya Jumanne. Mvua kubwa inaendelea katika eneo lote, na vifo vimeripotiwa tayari nchini Haiti, Jamhuri ya Dominika, na Jamaica.
Bi. Fontan ameeleza kuwa kimbunga hicho kitaleta mvua mara tatu zaidi ya kiwango cha kawaida cha mwezi wa msimu wa mvua nchini Jamaica hadi kufikia milimita 700.
“Hii inamaanisha kutakuwa na mafuriko ya ghafla ya kushtua na maporomoko mengi ya udongo,” amesema.
Amebainisha kuwa “Mbali na mvua na upepo wa maangamizi, kutakuwa pia na wimbi la bahari lenye urefu wa mita tatu hadi nne katika pwani ya kusini mwa Jamaica.”
Uharibifu mkubwa wa miundombinu unatarajiwa
Akizungumza kutoka Port of Spain, Trinidad na Tobago, Bwana. Mghendi amesema kwamba ingawa kimbunga Melissa kinasonga kwa kasi ndogo sana takribani kilomita sita kwa saa “mvua na upepo wa kiwango cha juu sana” vinatarajiwa kusababisha “uharibifu mkubwa wa miundombinu, kutenga jamii, na kukatiza huduma muhimu kwa siku au hata wiki.”
“Tishio la kibinadamu ni kubwa na la haraka,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa familia nyingi bado zinajenga upya maisha yao kutokana na Kimbunga Beryl cha mwaka jana.
Ameonya kuwa “Melissa sasa inatishia jamii hizo hizo, na huenda shughuli zote zikafutika”.
Bwana. Mghendi aliongeza kuwa jamii za pwani zinakabiliwa na changamoto za kifedha, na makazi yasiyo rasmi yako katika hatari kutokana na upepo mkali na udongo uliojaa maji, “unaoweza kusababisha maporomoko ya ardhi.”
Wafanyakazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani wajadili usambazaji wa misaada katika ghala moja nchini Jamaica.
Vipaumbele: Kuokoa maisha
Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na misaada ya Dharura (OCHA), Jens Laerke, amesema kuwa “kipaumbele cha kwanza ni kuokoa maisha kadri iwezekanavyo,” akifafanua kuwa ndiyo sababu “uhamishaji wa watu unaendelea, makazi ya muda yanajengwa, na tahadhari zinatolewa.”
Bwana. Mghendi amesema kuwa serikali ya Jamaica imeandaa takriban vituo 800 vya makazi ya dharura, na kwamba wahisani wa IFRC wanasaidia katika uhamishaji, kusambaza misaada na kuimarisha ujumbe wa tahadhari za mapema.
Msaada wa dharura waanzishwa kwa Cuba na Haiti
Bwana. Laerke ameongeza kuwa mfumo wa uangalizi wa mapema wa Umoja wa Mataifa umeanzishwa Cuba na Haiti nchi zilizoko kwenye njia ya kimbunga hicho na umechochea mchango wa dola milioni 4 kutoka Mfuko wa Dharura wa Kati wa Umoja wa Mataifa CERF ili kuandaa chakula, maji safi, vifaa vya usafi na huduma za afya kabla ya dharura.
Amesema “Kipaumbele ni mahitaji ya msingi ya watu kama chakula, maji safi, makazi, na huduma za afya.”
Pia amesema “Mafuriko makubwa yakitokea, upatikanaji wa maji safi hupungua, na hatari za kiafya na milipuko ya magonjwa huongezeka.”
Wito wa mshikamano wa dunia
Bwana. Mghendi amesema kuwa Jamaica ina vifaa vya misaada vya kutosha kusaidia kaya 800 mara moja, na kwamba vifaa vya kusaidia kaya 60,000 vinaweza kusafirishwa kwenda Jamaica na nchi nyingine kama Bahamas ndani ya saa nne.”
Amesisitiza kuwa “Baada ya kuvitumia, tutahitaji kujaza upya, na hapa ndipo tunapotarajia mshikamano wa dunia”.
Amehitimisha kwa kusema kuwa “Katika matukio kama haya, dunia huungana, na naamini itakuwa hivyo. Hiki ni moja ya vimbunga vikubwa vya karne hii, na jamii ya kimataifa italazimika kushirikiana kukabiliana nacho”.