Maswa. Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imetoa mikopo yenye thamani ya Sh124.1 milioni kwa vikundi 39 vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu, katika utekelezaji wa agizo la Serikali la kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya makundi haya maalumu.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mikopo hiyo leo Oktoba 28,2025  Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano amewataka wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa na kurejesha kwa wakati, ili iweze kunufaisha makundi mengine.

Amesema kuwa licha ya nia nzuri ya Serikali ya kuwakomboa wananchi wake kiuchumi kupitia mikopo hiyo, lakini wapo ambao wanadhani fedha hizo ni za bure na hazina mwenyewe.

“Serikali imeweka fedha hizi kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kiuchumi. Kila mkopaji anatakiwa kuwa mwaminifu na kurejesha fedha kwa wakati. Tunataka fedha hizo ziwanufaishe na wengine,” amesema.

Amesema kuwa licha ya mikopo hiyo kuwa ni  fursa muhimu ya kuinua kipato cha wananchi, kundi la vijana limekuwa likiongoza kwa kushindwa kurejesha mikopo waliyopewa katika miaka iliyopita.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano (wa pili kushoto) akikabidhi mfano wa hundi ya mkopo kwa  wawakilishi wa vikundi vya vijana wilaya ya Maswa. Picha na Samwel Mwanga

“Takwimu zinaonesha vijana wamekuwa wakirudisha mikopo kwa kusuasua, jambo ambalo halikubaliki. Nawaomba mbadilike, muoneshe mfano bora katika nidhamu ya kifedha,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, amesema kati ya kiasi hicho cha mikopo, vikundi 31 vya wanawake vimepatiwa Sh97.8 milioni, vikundi saba vya vijana vimepewa Sh21.3 milioni,  huku kikundi kimoja cha watu wenye ulemavu kikipatiwa Sh5 milioni.

Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wameeleza furaha yao na kuahidi kuitumia kwa uadilifu ili kuleta tija katika shughuli zao.

Zaituni Magesa, Mwenyekiti wa kikundi cha wanawake cha Upendo Group kilichopata mkopo wa Sh4 milioni, amesema fedha hizo zitawasaidia kununua mbegu bora za pamba na kupanua mashamba yao.

“Tulikuwa tunahangaika kupata mtaji wa kuendeleza kilimo chetu, sasa tunashukuru Serikali kwa kutuamini. Tutaweka nguvu kuhakikisha tunarejesha fedha kwa wakati,” amesema.

Naye John Elias ambaye ni mwakilishi wa vijana wa Ushirikiano Group, amesema mkopo waliopata utawasaidia kununua vifaa vya kilimo na kukodisha maeneo kwa ajili ya kilimo.

“Tunalima pamba na mpunga, fedha hizi zitatupa uwezo wa kutumia teknolojia ya kisasa na kuongeza uzalishaji. Tunatambua wajibu wa kurejesha fedha hizi kwa wakati,” amesema.

Kwa upande wake, Neema Joseph, mwakilishi wa watu wenye ulemavu  amesema wamepanga kutumia mkopo wao wa Sh5 milioni  kuanzisha kilimo cha mbogamboga.

“Huu ni mwanzo mzuri kwa watu wenye ulemavu kujitegemea. Tunataka kuonesha kuwa tunaweza kuzalisha na kuchangia uchumi wa Maswa,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *