London, England. Imechezwa michezo tisa pekee ya Ligi Kuu England msimu huu, lakini tayari presha imeanza kuwapanda baadhi ya makocha, huku wengine wakianza kunusurika baada ya matokeo mazuri ya hivi karibuni.
Ligi hiyo maarufu duniani kwa mzunguko wa makocha inaendelea kuwageuza majemedari kuwa waathirika wa mapema. Tayari makocha watatu Graham Potter, Nuno Espirito Santo na Ange Postecoglou wameshatimuliwa, ingawa msimu bado uko hatua za mwanzo.
Hata hivyo, hali hiyo haijawazuia baadhi ya makocha wengine kuanza kuhisi joto, huku wengine wakiwa salama kabisa kutokana na matokeo mazuri ya timu zao.
Walioko salama
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, hana cha kuhofu baada ya kuongoza timu yake kileleni mwa msimamo. Vilevile, Andoni Iraola (Bournemouth), Regis Le Bris (Sunderland) na Thomas Frank (Tottenham Hotspur) wote wanaendelea vizuri.
Kwa upande wa Manchester City, Pep Guardiola bado ndiye mwenye maamuzi juu ya mustakabali wake, na hakuna dalili za kutimuliwa. Oliver Glasner naye anaonekana salama baada ya kuipa Crystal Palace Kombe la FA msimu uliopita, huku Sean Dyche akiwa ameandika mwanzo mzuri Nottingham Forest kwa ushindi kwenye mechi yake ya kwanza.
Wasiokuwa hatarini sana
Msimu ulipoanza, haingeingia akilini kusema kuwa Arne Slot angeingia kwenye presha Liverpool. Lakini sasa hali si shwari.
Majogoo wa Anfield wamepoteza mechi tano kati ya sita, na matumaini ya kutwaa taji yameanza kufifia. Ingawa hakuna taarifa rasmi za kumtaka aondoke, mashabiki wanataka kuona timu ikirejea kwenye kiwango chake.
Hali kama hiyo pia ipo kwa Unai Emery (Aston Villa), Enzo Maresca (Chelsea) na Eddie Howe (Newcastle), ambao bado wako salama, lakini matokeo mabaya yanaweza kubadilisha hali hiyo.
Makocha kama Scott Parker, David Moyes, Daniel Farke, Keith Andrews na Fabian Hürzeler kwa sasa wako upande salama lakini si sana.
Walioko nusu hatarini
Ruben Amorim alikuwa miongoni mwa makocha waliokuwa kwenye hatihati wiki chache zilizopita akiwa na Manchester United, lakini matokeo mazuri ya karibuni yamepunguza presha kwake. Hata hivyo, wingu la hofu bado halijaondoka kabisa kichapo kingine kinaweza kumrudisha pabaya.
Marco Silva wa Fulham naye anakabiliwa na presha ndogo baada ya mwanzo hafifu wa msimu wenye ushindi mechi mbili pekee.
Huko London, Nuno Espirito Santo, ambaye tayari alitimuliwa Nottingham Forest, sasa yuko West Ham bila ushindi hata mmoja, hali inayoweza kumgharimu tena nafasi yake.
Wako njia panda
Kwa Vitor Pereira wa Wolves, hali ni mbaya zaidi. Kukabiliana na mashabiki kwa hasira baada ya kupoteza mechi ya mwisho dhidi ya Burnely kumeibua dalili za presha kuhusu hatma yake.
Ripoti zinaeleza kwamba uongozi wa Wolves unaweza kufanya uamuzi wa kumtimua kabla ya wiki hii kumalizika ikiwa timu itapoteza tena mwishoni mwa wiki.