
Waziri wa Afya katika jimbo la Darfur, Babiker Hamdeen amesema kwamba maelfu ya raia wameuawa katika mji wa El Fasher katika siku mbili zilizopita, huku Umoja wa Afrika ukilaani “ukatili” na “madai ya kufanyika uhalifu wa kivita” huko El Fasher, magharibi mwa Sudan.
Waziri huyo amesema kuwa idadi kamili ya waliouawa haikuweza kubainika kutokana na kukatika mawasiliano, na kwamba wale waliofanikiwa kutoka nje ya mji huo wamethibitisha vifo vya maelfu huko El Fasher.
Wakati huo huo vyanzo vya kimatibabu vimethibitisha kuwasili katika mji wa Tawila familia zaidi ya 100 zilizokimbia vita. Vilevile, Madaktari Wasio na Mipaka wametoa wito wa kuokolewa maisha ya raia huko El Fasher na kuruhusiwa kuondoka na kuelekea kwenye maeneo salama zaidi.
Haya yanajiri huku Malik Agar, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Sudan, akisema, hii leo Sudan unapita katika kipindi kigumu, lakini sio mwisho wa safari. Agar ameonya kwamba kurudi nyuma kwa jeshi katika mapigano huko “El Fasher kunawataka Wasudani wote kuungana.”
Ripoti za uwanjani zilizotolewa leo Jumanne zinaonyesha kuwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vimetekeleza mauaji makubwa ya raia huko El Fasher na kuwateka nyara madaktari kadhaa baada ya kudhibiti mji huo, ambao ulikuwa ukizingirwa kwa miezi kadhaa.
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf amelaani “ukatili” na “uhalifu wa kivita” ulioripotiwa katika mji wa El Fasher nchini Sudan.
Kwa upande wake, Mamlaka ya Maendeleo ya Serikali Mbalimbali (IGAD) imeeleza wasiwasi wake kuhusu hali inayozidi kuwa mbaya huko El Fasher baada ya mji huo kutwaliwa na Vikosi vya Msaida wa Haraka. IGAD pia imelaani ukatili unaofanyika dhidi ya raia, ikitaka kusitishwa mara moja kwa uhasama.