MTIBWA Sugar ina takribani siku 28 kutoka leo Oktoba 28, 2025 hadi Novemba 25, 2025 kujitetea ili kuepuka kushushwa daraja kwa mujibu wa Kanuni ya 47:19 za Ligi Kuu Bara toleo la mwaka 2025.

Leo Oktoba 28, 2025, Mtibwa Sugar imepigwa faini ya jumla Sh20 milioni na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), kwa kosa la kuanza msimu wa Ligi Kuu Bara na kucheza mechi nne bila kuwa na kocha mkuu mwenye ujuzi kwa mujibu wa Kanuni ya 77:33 (1,2,3).

Muda mchache baada ya kupigwa faini hiyo, ikashuka dimbani katika mechi ya tano ikiwa bado inafundishwa na Awadh Juma, ambaye kikanuni hakidhi vigezo vya kuwa kocha mkuu wa timu inayoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu kwa mujibu wa Kanuni ya 77:33 (1,2,3).

Adhabu ya Mtibwa Sugar imetolewa kwa mujibu wa Kanuni Kanuni ya 47:19 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Kanuni hiyo ya 47:19 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu, inasema: “Timu yoyote ya Ligi Kuu itakayoanza msimu mpya na kucheza mchezo wa Ligi bila kuwa na kocha mwenye ujuzi kwa kanuni ya 77: (1,2,3) itatozwa faini ya shilingi milioni tano (5,000,000) kwa kila mchezo kwa michezo mpaka sita (6) ya Ligi Kuu, endapo bado itashindwa kutimiza sharti hili la kuwa na kocha anayehitajika kikanuni, itaondolewa kwenye Ligi Kuu na kushushwa daraja.”

Kwa maana hiyo, Mtibwa Sugar ambayo leo Oktoba 28, 2025 imecheza mechi ya tano ya ligi dhidi ya Yanga huku ikiendelea kuongozwa na Kocha Awadh Juma ambaye hajakidhi vigezo vya kusimama kama kocha mkuu, imebakiwa na mechi moja dhidi ya KMC itakayochezwa Novemba 25, 2025 kufika sita. Hadi kufikia hapo ikiwa haijakidhi vigezo vya kuwa na kocha mkuu, itashushwa daraja kwa mujibu wa kanuni.

Mechi ilizocheza Mtibwa hadi sasa ni tano ikishinda moja, sare mbili na kupoteza mbili. Mechi hizo ni dhidi ya Mashujaa (Septemba 21, 2025), Fountain Gate (Septemba 28, 2025), Costal Union (Oktoba 19, 2025), Dodoma Jiji (Oktoba 22, 2025) na Yanga (Oktoba 28, 2025).

Mtibwa imerejea Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kushuka daraja 2023-2024 , hivyo msimu uliyopita ilicheza Ligi ya Championship.

Alipotafutwa Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru amesema tayari klabu hiyo ipo kwenye mchakato wa kukamilisha ujio wa kocha mpya.

“Tunafanya mchakato wa kumleta kocha ndani ya wiki hii au ijayo, tumemalizana naye kila kitu, hivyo hilo lipo ndani ya uongozi,” amesema Kifaru.

Kifaru ameongeza: “Adhabu tuliyopewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania imetusisitiza jambo ambalo tunatakiwa kulifanyia haraka.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *