
Dar es Salaam. Baada ya kusimamia kwa siku moja mazoezi ya Yanga, kocha mkuu wa timu hiyo, Pedro Goncalves leo anakutana na kipimo cha kwanza ambacho ni mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Goncalves alijiunga rasmi na Yanga, Jumamosi iliyopita akichukua nafasi ya Romain Folz ambaye alifikia makubaliano ya kuachana na Yanga baada ya timu hiyo kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Silver Strikers ya Malawi katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Oktoba 18, 2025.
Na muda unaonekana kuwa ni mchache kwa Goncalves kwani leo atakuwa na jukumu la kuhakikisha Yanga inaondoka na pointi tatu katika mchezo muhimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex kuanzia saa 10:00 jioni.
Yanga inaingia uwanjani leo ikiwa tayari imecheza mechi mbili za ligi msimu huu na kukusanya pointi nne kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji na matokeo ya 0-0 dhidi ya Mbeya City.
Rekodi zinaonesha katika mechi kumi za Ligi Kuu zilizopita dhidi ya Mtibwa Sugar, Yanga imeshinda nane, sare moja na kupoteza moja. Mara ya mwisho Yanga kupoteza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar ilikuwa Aprili 17, 2019, baada ya hapo, imeshinda tisa na sare moja. Katika ushindi wa mechi hizo tisa, nane ni mfululizo.
Licha ya uimara wa Yanga, ila ni wazi kwamba safu ya ulinzi ya Mtibwa ni ngumu kufunguka kwani imeruhusu bao moja tu katika mechi nne ilizocheza msimu huu ikirejea Ligi Kuu Bara.
Yanga katika mchezo wa leo, Yanga inaweza kumtumia mshambuliaji wake Clement Mzize ambaye alikosa mchezo uliopita kutokana na majeraha.
“Mzize (Clement) alijitonesha, hivyo bado hayuko sawa na mpaka baadae tutajua kama yupo au la, Ecua (Celestine) pia yuko salama, yuko nje tu kwa maswala ya kiufundi.
“Kama mechi ya kesho (leo) itamuhitaji basi kocha atampanga na mashabiki watamuona tena kwani jamaa yuko vizuri kwa ajili ya kazi,” amesema Kamwe.
Kocha wa Mtibwa Sugar, Awadh Juma amesema kuwa wanatambua wanakutana na timu kubwa hivyo wanaamini wanatakiwa kuwa makini.
“Kabla hujacheza utakuwa unahitaji matokeo. Presha tuliyonayo ni vipi tunakwenda kupata pointi kwa Yanga. Yanga ni timu kubwa sio tu Tanzania bali katika Bara la Afrika,” amesema Juma.