
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani uchochezi wa kijeshi wa Marekani kandokando ya Venezuela ikisema ni tishio kwa amani na usalama katika eneo la Karibi na Amerika Kusini.
Akizungumza katika mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari mjini Tehran jana ya Jumanne, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Iran, Esmaeil Baqaei alilaani uchochezi wa kutisha wa Marekani unaolenga taifa hilo la Amerika Kusini na kuutaja kuwa ni kielelezo cha “sera za Washington za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja katika ngazi ya kimataifa.”
“Sheria muhimu zaidi za kimataifa zinakataza matumizi ya nguvu na zinahimiza kuheshimiwa uhuru wa kujitawala wa nchi mbalimbali,” amesema Esmaeil Baqaei.
Matamshi hayo yanafuatia ongezeko kubwa la harakati za kijeshi za Marekani dhidi ya Venezuela, ikiwa ni pamoja na kutuma meli na ndege za kijeshi karibu na nchi hiyo.
Tangu mwezi Septemba, Marekani imefanya mashambulizi 10 dhidi ya meli zinazodaiwa kuwa za biashara haramu ya dawa za kulevya katika eneo la Karibi, na kutuma meli za kivita, ndege zisizo na rubani, na ndege za kivita, katika eneo hilo ikiwemo meli kubwa ya kubeba ndege ya kivita ya USS Gerald R. Ford.
Venezuela imezitaja hatua hizo kuwa ni uchochezi wa Marekani unaolenga kuipindua serikali ya Rais Nicolas Maduro iliyochaguliwa kidemokrasia nchini humo.