
KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Oktoba 27, 2025, imefikia uamuzi wa kuipa Pamba Jiji pointi tatu na mabao matatu kutokana na mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji wao, Dodoma Jiji kushindwa kuendelea.
Taarifa iliyotolewa leo Oktoba 28, 2025 na Idara ya Habari na Mawasiliano ya TPLB, imesema kamati hiyo katika kikao chake hicho ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya uamuzi kwa matukio ya mechi mbalimbali zilizochezwa ikiwemo hiyo ya Oktoba 25, 2025.
“Klabu ya Pamba Jiji imepewa ushindi wa mabao matatu (3) na pointi tatu (3) huku klabu ya Dodoma Jiji ikipoteza mchezo kwa kosa la klabu hiyo iliyokuwa mwenyeji kushindwa kuandaa mchezo huo kikamilifu, jambo lililosababisha mchezo kuvurugika kabla ya kuvunjwa kwa mujibu wa Kanuni ya 32:1 ya Ligi Kuu kuhusu Kuvuruga Mchezo.
“Mchezo huo ulilazimika kusimama katika dakika ya sita (6) Dodoma Jiji ikiongoza kwa bao 1-0, baada ya taa za uwanja wa Jamhuri kuzimika na klabu hiyo kushindwa kufanya jitihada zozote za kurejesha mwanga uwanjani hapo ili mchezo uendelee.
“Kutokana na adhabu hiyo na kwa mujibu wa Kanuni ya 32:3 ya Ligi Kuu kuhusu Kuvuruga Mchezo, bao hilo lililofungwa na mchezaji Benno Ngassa wa Dodoma Jiji limefutwa, hivyo halitahesabiwa kwenye orodha ya mabao ya mchezaji huyo wala ya klabu ya Dodoma Jiji,” imeeleza taarifa hiyo.
Kutokana na Pamba Jiji kupewa pointi tatu za mechi hiyo, sasa imefikisha pointi nane na kupanda kutoka nafasi ya kumi hadi ya pili, ikiwa sawa na kinara Mbeya City na Mashujaa iliyo nafasi ya tatu.