Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ametoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya ECO kuanzisha na kutekeleza mfumo thabiti wa usalama, unaounda utulivu, wa ndani, na unaozingatia maendeleo.
Akizungumza leo katika Mkutano wa Nne wa Mawaziri wa ECO mjini Tehran, Rais Pezeshkian amelitaja shirika hilo kuwa ni mrithi wa miongo kadhaa ya juhudi, ushirikiano na utendaji wa wanachama wake kwa ajili ya muungano wa kiuchumi.
“Mafanikio katika ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda yanahitaji, miongoni mwa mambo mengine, mifumo na majukwaa ya pamoja, imara, yanayotabirika, thabiti na yanayostahimilika,” amesema Rais Pezeshkian.
Vilevile amezihimiza nchi za Asia ya Kati, Caucasus, Asia Kusini, Asia Magharibi na Ghuba ya Uajemi, ikiwa ni pamoja na nchi wanachama wa ECO, “kuanzisha na kutekeleza usanifu thabiti wa usalama, imara wa ndani na unaozingatia maendeleo.”
Jumuiya ya ECO Iliyoanzishwa mwaka wa 1985 na Iran, Uturuki, na Pakistan, imepanuka hadi kujumuisha Afghanistan, Azerbaijan, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan, Turkmenistan na Uzbekistan. Hii leo, jumuiya hiyo inatumika kama jukwaa kuu jumuishi wa kiuchumi la kikanda.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Rais Pezeshkian amesema kwamba mataifa ya eneo hilo ni “jukwaa muhimu la mazungumzo, kubadilishana uzoefu na ushirikiano katika nyanja zote.”
Amesema: Miongoni mwa kazi ambazo hazijakamilika katika jumuiya ya ECO ni kuundwa kikosi cha polisi cha ECO kinachoitwa ECOPOL, ambacho mchakato wake bado haujakamilika.”
Rais Pezeshkian amesema, eneo la ECO ni “mojawapo ya maeneo machache duniani ambayo hayana kikosi cha pamoja cha polisi.”
“Eneo letu na maeneo yanayolizunguka hayana kinga ya mashambulizi ya kigeni,” na kuongeza kuwa uingiliaji kati mkubwa zaidi wa kigeni katika historia ya kisasa umefanyika katika eneo hili.
Akizungumzia uvamizi wa Israel huko Palestina, Pezeshkian amesema kwamba “uvamizi mkubwa zaidi wa karne hii” unaendelea karibu na eneo letu baada ya takriban miongo 8.
“Mauaji ya kimbari na uhalifu mbaya zaidi dhidi ya ubinadamu duniani umefanywa na utawala ghasibu wa Israel katika eneo la Asia Magharibi katika miaka miwili iliyopita,” ameongeza Rais wa Iran na kuonya kwamba “kuna kiu kubwa miongoni mwa watu wenye msimamo mkali wa kimataifa na wanaovunja sheria kwa ajili ya uwepo na kuingilia masuala ya eneo letu na maeneo ya pembezoni.”