London, England. Nahodha wa zamani wa Manchester United, Wayne Rooney, ametoa onyo kali kwa kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, akisema kama ataacha ubingwa wa Ligi Kuu England utoroke tena msimu huu, basi huenda klabu ikaamua kumtimua.
Arsenal kwa sasa inaongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi nne baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Crystal Palace, huku wapinzani wao wakipoteza pointi mwishoni mwa wiki. Ni ushindi wa nne mfululizo kwa vijana wa Arteta, ambao sasa wamejikita kileleni kama vinara wa ligi.
Hata hivyo, Rooney amesema kuwa kutokana na nafasi nzuri waliyonayo, mashabiki na uongozi wa Arsenal hawatakubali kuona taji hilo likipotea tena.
“Arsenal wana kikosi kizuri sana na kocha mzuri. Arteta amekuwa karibu mara kadhaa. Wamekusanya pointi nyingi ambazo katika misimu mingine zingetosha kubeba ubingwa,” amesema Rooney.
“Sasa ana kikosi ambacho kinatarajiwa kushinda ligi. Wana nguvu, wana nidhamu ya kiufundi na wana safu bora ya ulinzi. Wamekuwa timu inayojua kusaka matokeo. Sasa presha ipo unaweza kuwa kileleni na kubaki hapo hadi mwisho?”
Rooney aliendelea:
“Nadhani wanaweza. Wamekomaa na wana uzoefu wa kukaribia mafanikio. Lakini msimu huu hakuna visingizio. Kama hawatabeba taji, naamini kutakuwa na mabadiliko ya kocha.”
Tangu ajiunge na Arsenal mwishoni mwa mwaka 2019, Arteta amefanikiwa kushinda Kombe la FA pekee, licha ya kutumia fedha nyingi kwenye usajili na kuungwa mkono na uongozi kila msimu.
Hata hivyo, mashabiki wamekuwa wakimlaumu kwa kushindwa kumalizia mbio za ubingwa licha ya kuongoza ligi kwa muda mrefu kama ilivyotokea misimu ya 2022/23 na 2023/24, ambapo Manchester City ilipora ubingwa mwishoni.
Arsenal haijawahi kutwaa taji la Ligi Kuu tangu ilipofanya hivyo mwaka 2004, lakini msimu huu ina nafasi kubwa ya kuvunja ukame huo ingawa, kama Rooney anavyosema, “ikishindikana safari hii, huenda pazia likamfungia Arteta.”