Wanaakiolojia nchini Senegal wamegundua ushahidi mpya wa mauaji ya kikoloni ya Ufaransa yaliyotokea mwaka 1944, kama sehemu ya juhudi zinazoongozwa na serikali za kufichua ukweli kuhusu mauaji yaliyofanywa na vikosi vya jeshi la Ufaransa baada ya Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya ya wanajeshi wa Afrika Magharibi.

Makaburi ya kijeshi ya Thiaroye, yaliyo karibu na mji mkuu wa Dakar, kwa sasa ndiyo kitovu cha uchimbaji mkubwa wa akiolojia unaolenga kutambua mabaki ya miili ya wanajeshi wanaodaiwa kuuawa na wakoloni wa Ufaransa mnamo Desemba 1, 1944.

Tukio hilo lilitokea baada ya karibu wanajeshi 1,600, wengi wao wakiwa ndio kwanza walikuwa wameachiliwa huru baada ya kutekwa na Wajerumani, kufikishwa kwenye kambi ya wakimbizi huko Thiaroye na kuanza kupinga kitendo cha kuzuiliwa mishahara yao na mienendo isiyo ya haki na usawa.

Wanajeshi wa Ufaransa waliwamiminia risasi wanaume hao, lakini idadi ya waliouawa na mazingira halisi ya tukio hilo vimeendelea kuzusha hitilafu kwa muda mrefu. Taarifa rasmi za enzi ya ukoloni wa Ufaransa nchini humo zilidai kuwa watu 70 waliuawa katika tukio hilo, lakini watafiti wa Senegal wanasema idadi na waliouawa inaweza kuwa kati ya 300 na 400.

Wanaakiolojia wamechimba makaburi saba katika kundi la awali la makaburi 34, na kupata mifupa mizima na sehemu za baadhi ya mifupa ya wengine. Kwa mujibu wa mwanaakiolojia Moustapha Sall, moja ya mifupa hiyo ilipatikana ikiwa na risasi karibu na moyo. Mingine ilionyesha dalili za majeraha, ikiwa ni pamoja na kutoweka uti wa mgongo, mbavu na mafuvu. Baadhi ya mabaki yaligunduliwa yakiwa na minyororo ya chuma kwenye miguu yao.

“Hii ina maana kwamba waliteswa kabla ya kuuawa,” amesema Sall na kuongeza kuwa “mojawapo ya dhana zilizopo ni kwamba makaburi haya yalitengenezwa baada ya mazishi ya awali, au kwamba yalipangwa ili ionekane kama wamezikwa ipasavyo.”

Kanali Saliou Ngom, mkurugenzi wa kumbukumbu za jeshi na urithi wa kihistoria wa Senegal, amesema kazi hiyo inalenga kufidia mapengo ya kihistoria yaliyosababishwa na kushindwa kupata kumbukumbu za kikoloni za Ufaransa.

Rais Bassirou Diomaye Faye wa Senegal ameidhinisha kuendelea kwa uchimbaji huo katika maeneo yote yanayoshukiwa kuwa na makaburi ya pamoja ya Wasenegali waliouawa na wakoloni wa Kifaransa.

“Matokeo ya awali hayajibu maswali yote,” amesema Rais Sall na kueleza kuwa “Lakini ni hatua muhimu sana katika utafutaji wa ukweli wa kihistoria.”

Mnamo Novemba 2024, wakati wa kumbukumbu ya miaka 80 ya mauaji Thiaroye, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikiri hadharani kwa mara ya kwanza kwamba wanajeshi wa kikoloni wa nchi yake walifanya “mauaji makubwa” katika eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *