Kikosi cha Simba kimetua Tabora leo saa 8 mchana tayari kwa mchezo wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya TRA United, Alhamisi, Oktoba 30, 2025.

Mchezo huo utachezwa katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, kuanzia saa 10:00 jioni kwa muda wa Afrika Mashariki.

Simba imetua Tabora ikiwa na rekodi nzuri ya ubabe dhidi ya wenyeji wao TRA United ambao zamani walikuwa wakijulikana kama Tabora United.

Katika mechi nne ambazo zimewakutanisha timu hizo katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba imepata ushindi mara zote huku TRA United ikiambulia patupu.

Sio tu kutopata ushindi, bali pia TRA United haijawahi kufunga hata bao katika mechi dhidi ya Simba, mara nne zote ambazo timu hizo zimewahi kukutana.

Msimu uliopita, katika mchezo wa kwanza ambao Simba ilikuwa nyumbani, iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya TRA United na ziliporudiana, Simba ikapata ushindi wa mabao 3-0.

Msimu wa 2023/2024, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 katika mechi ya kwanza na ziliporudiana, Simba ikaibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Msimu huu zinakutana huku Simba ikiwa imepata ushindi katika mechi zake mbili za mwanzo dhidi ya Fountain Gate na Namungo FC wakati huo TRA United ikiwa imetoka sare tatu dhidi ya Dodoma Jiji, Pamba Jiji FC na Mashujaa FC.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *