Dar es Salaam. Kocha mpya wa Yanga, Pedro Goncalves ameanza kazi kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa leo kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
Goncalves raia wa Ureno ambaye alitambulishwa ndani ya Yanga Oktoba 25, 2025, hii ilikuwa mechi yake ya kwanza na mwanzo wake umekuwa mzuri ambapo alishuhudia vijana wake, Mohamed Hussein na Celestine Ecua wakifunga mabao hayo.
Dakika ya 39, beki wa Yanga, Mohamed Hussein alipiga shuti akiwa nje ya 18 wakati kipa wa Mtibwa Sugar, Costantine Malimi akashindwa kuokoa na kujikuta akiusindikiza mpira nyavuni. Bao ambalo liliamsha shangwe la mashabiki waliojitokeza uwanja.
Baada ya bao hilo, wachezaji wa Yanga walianza kupiga mashuti ya mbali wakijaribu bahati ya kuongeza mengine.
Kwa asilimia kubwa, kipindi cha kwanza Mtibwa Sugar ilijitahidi kuzuia mashambulizi ya Yanga licha ya kuruhusu bao moja, huku eneo la kiungo kwa kila timu likiwa imara.
Katika kipindi hicho cha kwanza, Yanga ilipiga mashuti 13, huku manane yakilenga lango, Mtibwa ilipiga mashuti manne, matatu yalilenga lango.
Bao la pili la Yanga lilifungwa na Celestine Ecua dakika ya 83 ambapo mchezaji huyo aliingia kuchukua nafasi ya Edmund John.
Kabla ya bao hilo, Yanga ilicheza ndani ya 18 ya Mtibwa Sugar takribani dakika tatu na kuipa presha safu ya ulinzi ya Mtibwa.
Kikosi cha Yanga:
Djigui Diarra, Bakari Mwamnyeto, Mohammed Hussein, Dickson Job, Maxi Nzengeli, Duke Abuya, Edmund John, Mohamed Doumbia, Prince Dube, Offen Chikola na Israel Mwenda.
Kikosi cha Mtibwa:
Constantine Malimi, Erick Kyaruzi, Haroun Evod, Omar Selemani, Ibrahim Imoro, Kassim Msafiri, Twalibu Muhenga, Omary Marungu, Abdul Hilary, Datius Peter na Nassor Kiziwa.