TIMU ya Taifa ya Soka ya Wanawake ya Tanzania, Twiga Stars, imefuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 baada ya kuiondosha Ethiopia kwa jumla ya mabao 3-0.

Twiga Stars imefuzu michuano hiyo baada ya leo Oktoba 28, 2025 kushinda bao 1-0, mechi ya marudiano dhidi ya Ethiopia iliyochezwa Uwanja wa Kimataifa wa Dire Dawa uliopo katika Jiji la Dire Dawa, Ethiopia. Awali ilishinda 2-0 nyumbani.

Katika mechi ya leo, Diana Lucas ndiye aliyefunga bao hilo pekee la ushindi dakika ya 15 akimalizia pasi ya nahodha wa kikosi hicho, Opa Clement.

KIKA 03

Bao hilo lilianzia nyuma kwa Christer Bahera aliyepiga mpira mrefu baada ya kutokea faulo, akauwahi Opa Clement, akamuachia Diana Lucas, akampasia Donisia Minja ambaye akampa Opa aliyeingiza krosi ya chini iliyomkuta Diana Lucas akatikisa nyavu.

Kuingia kwa bao hilo, kukazidisha ushindani huku wenyeji wakiamka wakipambana kusaka bao la kusawazisha ili kutafuta nafasi ya kupindua matokeo na kufuzu, lakini safu ya ulinzi ya Twiga Stars ikiwa na nyota kama Anastazia Katunzi na Julitha Singano ilikaa imara kuzima mashambulizi.

Hadi filimbi ya mwisho inapulizwa, Twiga Stars imeondoka uwanjani ikiwa na furaha kutokana na kufuzu WAFCON 2026, ikiwa ni mara ya tatu katika historia ya timu hiyo baada ya 2010, michuano iliyofanyika Afrika Kusini na 2024, michuano iliyochezwa mwaka 2025 nchini Morocco.

Twiga Stars imefuzu WAFCON 2026 kwa jumla ya mabao 3-0, kufuatia mechi ya kwanza iliyochezwa Oktoba 22, 2025 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kushinda 2-0, mabao yaliyofungwa na Aisha Mnunka na Jamila Rajab.

KIKA 02

Mara ya kwanza Twiga Stars kushiriki mashindano ya WAFCON mwaka 2010, iliishia hatua ya makundi ikipangwa Kundi A ambapo haikuambulia pointi katika mechi tatu ilizocheza, ikipoteza zote. Mwaka huo, timu nane zilishiriki ambapo Nigeria ikatwaa ubingwa.

Katika WAFCON 2024 iliyochezwa mwaka 2025 nchini Morocco, Twiga Stars ilishiriki kwa mara ya pili na kumaliza mkiani mwa Kundi C ikikusanya pointi moja, iliyotokana na kutoka sare moja na kupoteza mbili.

Kabla ya kuiondoa Ethiopia wakati wa kufuzu WAFCON 2026, Twiga Stars ilianza hatua ya kwanza kwa kuifunga Equatorial Guinea jumla ya mabao 4-2. Mechi ya kwanza Dar es Salaam ilishinda 3–1, kisha ugenini ikawa sare ya 1–1.

Mbali na Morocco ambayo ni timu mwenyeji iliyofuzu moja kwa moja, Twiga Stars imekuwa ya pili kufuzu WAFCON 2026 baada ya Zambia. 

Jumla ya timu 12 zinatarajiwa kushiriki mashindano hayo kuanzia Machi 17, 2025 hadi Aprili 3, 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *