Nairobi. Eric Ominde, aliyekuwa dereva wa hayati, Raila Odinga kwa zaidi ya miaka 20, amesimulia simu ya mwisho aliyopokea kutoka kwa kiongozi huyo maarufu wa upinzani kabla ya kifo chake cha ghafla.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha NTV Kenya jana Oktoba 27, 2025, Ominde amesema Raila alimpigia simu saa 7:00 usiku kwa saa za India, akiwa na ujumbe wa kumtia moyo.
“Aliniambia jitahidi uwe imara; nitakuja,’” amesema Ominde huku akionekana mwenye huzuni.
Raila Odinga alifariki dunia Oktoba 22, 2025, nchini India, alipokuwa akipatiwa matibabu, kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka kwa familia, kifo chake kilitokana na shambulio la moyo (cardiac arrest) lililotokea ghafla wakati akiwa chini ya uangalizi wa madaktari.
Kifo cha Waziri Mkuu huyo mstaafu kimeacha simanzi kubwa nchini Kenya na ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na mchango wake wa muda mrefu katika siasa, demokrasia, na harakati za haki za kijamii.
Wafuasi wake wengi wanamkumbuka kama ‘rais wa wananchi’ kutokana na ujasiri wake wa kupigania utawala bora.
Mazishi ya kiongozi huyo yalifanyika Oktoba 19, 2025, nyumbani kwake kijijini Bondo, Kaunti ya Siaya, kwa heshima za kitaifa.
Ominde (43), amemtaja Raila alikuwa kiongozi asiyechoka na mwenye moyo wa utu, akisema walishirikiana kwa karibu katika kampeni za kisiasa na shughuli za kiserikali.
Amesimulia kuwa alianza kumfanya kazi na Raila miaka ya 2000 baada ya kuajiriwa kama mfanyakazi binafsi wa kiongozi huyo.
Eric Ominde, aliyekuwa dereva wa hayati, Raila Odinga
“Niliondolewa kwenye msafara, kisha Baba akaniambia nibaki. Akaanza kunifundisha kazi yenyewe,” amesema Ominde.
Mwaka 2008, wakati wa Serikali ya Muungano, Raila alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu baadhi ya maofisa walipendekeza apewe dereva mpya, lakini Raila alikataa.
“Alimwambia Rais Mwai Kibaki na Francis Muthaura kwamba tumekuwa pamoja muda mrefu na lazima nibaki naye,” amesema.
Ominde anakumbuka pia siku za hatari, hasa Januari 30, 2018, wakati Raila alipojitambulisha kama ‘rais wa wananchi’.
“Niliendesha gari kutoka Karen hadi Uhuru Park, kisha tukapita kwa siri hadi Ukumbi wa Jiji. Mzee aliniambia nisiogope,” amesema kwa kumbukumbu.
Kwa sasa, Ominde anaendelea na kazi yake ya udereva Ikulu, lakini anasema kumbukumbu za miaka aliyoitumikia familia ya Raila zitabaki moyoni mwake milele.
Imeandikwa na Evagrey Vitalis kwa msaada wa Mashirika