Barcelona, Hispania. Nyota wa Barcelona, Lamine Yamal, anaelezwa kuwa na mpango wa kununua jumba la kifahari lililokuwa linamilikiwa na beki wa zamani wa klabu hiyo Gerard Piqué na mwanamuziki maarufu duniani Shakira.

Kwa mujibu wa gazeti la El País la Hispania, Yamal, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 18 na analipwa mshahara wa takribani pauni 325,000 ambazo ni zaidi ya Sh1 bilioni za Kitanzania kwa wiki, anataka kulimiliki jumba hilo lililoko katika eneo la kifahari jijini Barcelona.

Piqué na Shakira waliishi kwenye jumba hilo kwa miaka kadhaa kabla ya kutangaza kutengana mwaka 2022, baada ya kuwa pamoja kwa zaidi ya miaka 12.

Jumba hilo lilijengwa mwaka 2012 na lina nyumba tatu tofauti katika eneo lenye ukubwa wa zaidi ya mita za mraba 3,800. Awali lilikuwa likiuzwa kwa pauni milioni 12 (Sh39 bilioni) wakati wenzi hao walipotengana, lakini thamani yake imeshuka kwa kiasi kikubwa baada ya moja ya nyumba hizo tatu kuuzwa kivyake.

Kwa sasa, jumba hilo limebaki na nyumba mbili tu na lina thamani ya pauni milioni 10 (Sh33 bilioni) likiwa na vyumba sita vya kulala na vyumba vitano vya bafu, pia lina uwanja wa tenisi, mabwawa mawili ya kuogelea (ndani na nje), na studio ya kurekodia muziki.

Ripoti zinaeleza kuwa Yamal, licha ya kuvutiwa na bei ya sasa, anapanga kutumia kiasi kingine kikubwa kufanya ukarabati ili kulifanya jumba hilo liendane na ladha zake binafsi.

Mbali na hilo, inadaiwa kuwa nyota huyo chipukizi tayari ameshawanunulia nyumba mpya mama yake, baba yake na bibi yake, jambo linaloonyesha uhusiano wa karibu alionao na familia yake nje ya soka.

Aidha, Yamal amekuwa akionekana mara kwa mara na mpenzi wake mpya, Nicki Nicole, mwanamuziki kutoka Argentina mwenye miaka 25, ambaye amekuwa akihudhuria michezo yake katika uwanja wa Nou Camp msimu huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *