
Manchester, England. Meneja wa Manchester City, Pep Guardiola ameonyesha kutofurahishwa na ongezeko la matumizi ya mipira iliyokufa na ile ya kurusha katika Ligi Kuu England (EPL) msimu huu.
Guardiola amedai kuwa hilo linafanya safari nyingi za ugenini kuwa kama timu zinaenda kukabiliana na Stoke City ambayo ilikuwa ikisifika kwa kutegemea mashambulizi yatokanayo na mipira ya kutenga na kurusha.
Manung’uniko hayo ya Guardiola yamekuja katika kipindi ambacho takriban asilimia 19 ya mabao yote ya Ligi Kuu England msimu huu yametokana na kona ambayo ni karibu asilimia tano zaidi kuliko mwaka mwingine wowote.
Pamoja na Guardiola kusifika na misimamo yake ya kutaka kila kocha abakie na mipango yake binafsi ya kimbinu, maji yanaonekana kumfika shingoni na sasa amesema kuwa hafurahishwi na namna mbinu ya kutegemea mipira ya kurusha na iliyokufa kusaka mabao inavyozidi kushamiri.
“Nakumbuka nilipokuwa sipo, Stoke City. Je, unaikumbuka Stoke City walipokuwa wakitupia? Sasa ni timu zaidi na zaidi zinazofanya hivyo lakini wakati huo labda Stoke ilikuwa ubaguzi.
“Nakumbuka nilipokuwa Barcelona na Bayern Munich, Arsene Wenger alizungumza kuhusu kwenda kucheza Stoke City lakini sasa inatokea mara nyingi.
“Labda haikutokea nilipofika, labda (tu) huko Burnley, lakini sasa ni ukweli. Na unapaswa kuzingatia. Lakini bado nina ndoto ya kucheza,” amesema Guardiola.