Leo ni Jumatano tarehe 07 Jamadil Awwal 1447 Hijria sawa na Oktoba 29 mwaka 2025.

Tarehe 7 Jamadil Awwal miaka 1058 aliaga dunia qari na mtaalamu maarufu wa Hadithi, Ibn Ghalbun.

Msomi huyo wa Kiislamu alizaliwa mwaka 309 Hijria katika mji wa Halab (Aleppo) nchini Syria lakini akachaga maskani nchini Misri.

Ibn Ghalbun alijifunza qira ya Qur’ani na Hadithi kwa wanazuoni wa zama zake na kuwa mwalimu mahiri katika taaluma hizo. Mtaalamu huyo wa Hadithi wa Kiislamu alikuwa ya mitazamo mipya kuhusiana na elimu ya qiraa ya Qur’ani tukufu ambayo imeelezwa na mwanafunzi wake, Makki bin Abu Twalib katika kitabu cha al Kashf.

Vilevile alikuwa hodari na gwiji katika fasihi na mashairi ya lugha ya Kiarabu. Kitabu muhimu zaidi ya Ibn Ghalbun ni al Irshad kinachohusiana na visomo saba vya Qur’ani tukufu.   

Katika siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, mfumo wa utawala wa serikali ya jamhuri uliasisiwa nchini Uturuki kwa uongozi wa Rais Mustafa Kemal mashuhuri kwa jina la Ataturk.

Kemal Ataturk aliiongoza kidikteta nchi hiyo kwa muda wa miaka 15 na kufanya hujuma za kufuta sheria, nembo pamoja na matukufu ya Kiislamu na wakati huo huo, kueneza utamaduni na nembo za Kimagharibi nchini humo. Hata baada ya kufariki dunia kiongozi huyo aliyekuwa na uadui na Uislamu mnamo mwaka 1938, njama hizo dhidi ya Uislamu nchini Uturuki ziliendelezwa na wafuasi wake.

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita yaani tarehe 7 Aban mwaka 1305 Hijria Shamsia Ayatullah Sayyid Hassan Modarres aliyekuwa miongoni mwa wanazuoni na wanamapambano maarufu nchini Iran alinusurika jaribio la kuuawa.

Jaribio hilo lilifanywa na vibaraka wa Shah Reza Pahlavi aliyekuwa maarufu kwa udikteta, ukatili na upinzani mkubwa dhidi ya maulama wa Kiislamu. Uhasama wa utawala wa kifalme wa Pahlavi dhidi ya Ayatullah Modarres ulitokana na mchango mkubwa wa mwanazuoni huyo wa Kiislamu katika kuwaamsha wananchi na kufichua njama za utawala wa Kipahlavi na muungaji mkono wake yaani serikali ya Uingereza.

Kwa kipindi fulani Ayatullah Modarres alikuwa mwakilishi wa wananchi wa Tehran katika Bunge. Baada ya kunusurika kifo katika jaribio hilo Ayatullah Modarres alipelekwa uhamishoni kwa amri ya mfalme dikteta Reza Khan na muda mfupi baadaye aliuawa shahidi na vibaraka wa Shah. 

Sayyid Hassan Modarres

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, askari jeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walishambulia Peninsula ya Sinai iliyoko Misri.

Mashambulio hayo yalianza baada ya Rais wa wakati huo wa Misri, Gamal Abdul Nassir kutaifisha mfereji wa Suez. Siku mbili baada ya mashambulio hayo, Uingereza na Ufaransa zilipeleka majeshi yao pembezoni mwa mfereji huo kwa lengo la kuusaidia utawala ghasibu wa Israel.

Mnamo mwaka 1957 majeshi vamizi ya Ufaransa, Uingereza na utawala haramu wa Israel yaliondoka katika ardhi ya Misri kufuatia mashinikizo ya fikra za waliowengi, madola mengi ya Magharibi na upatanishi wa Umoja wa Mataifa.   

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, katika jinai yao nyingine, Wazayuni waliwauwa kwa umati wakazi wa kijiji cha Kafr Qasim huko Palestina.

Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni walitangaza utawala wa kijeshi katika kijiji hicho.

Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni waliwauwa kwa umati wanawaume, wanawake na watoto madhlumu wa Palestina wasiopungua 49 na kujeruhi makumi ya wengine huko Kafr Qasim.

Mauaji ya umati ya wakazi wa kijiji cha Kafr Qasim

Miaka 61 iliyopita katika siku kama ya leo tarehe 7 Jamadil Awwal Sayyid Qutb msomi na mwanamapambano wa Misri alinyongwa akiwa pamoja na wenzake wawili huko Cairo mji mkuu wa nchi hiyo.

Msomi huyo alihifadhi Qur’ani Tukufu katika ujana wake. Sayyid Qutb alifahamiana na Hassan al Bana na kujiunga na harakati ya Ikhwanul Muslimin ya nchi hiyo wakati alipokuwa katika harakati za kisiasa nchini Misri.

Sayyid Qutb alitiwa nguvuni na baadaye kunyongwa baada ya kuzuka hitilafu kati ya Gamal Abdel Nasser Rais wa wakati huo wa Misri na Ikhwanul Muslimin. Msomi huyo alikuwa akiamini kwamba “kambi za Mashariki na Magharibi zinapigana na Waislamu na kwamba kambi mbili hizo zimeungana ili kupora rasilimali za nchi za Kiislamu”.

Miongoni mwa vitabu vya msomi na mwanamapamban huyo wa Kiislamu ni “Fii Dhilalil Qur’an” na kile alichokipa jina la” Uislamu na Amani ya Kimataifa”.

Sayyid Qutb

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *