Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wadau wa muziki na wachambuzi wakidai kiwango cha msanii Alikiba kimeshuka hasa kimataifa, wengi wanasahau kuwa mwanamuziki huyo aliwahi kukinukisha katika upande huo.

Ally Saleh Kiba maarufu Alikiba, aliwahi kujitosa kimataifa na kufikia hatua ya kukutana na nguli wa R&B kutoka Marekani, R. Kelly, kupitia mradi wa kimuziki uliohusisha wasanii kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika. 

Mwaka 2010 King alifanikiwa kusafiri mpaka Chicago, Marekani ambapo alichaguliwa kuiwakilisha Tanzania kwenye ‘One8 Project’, kundi lililojumuisha wakali kama 2Face Idibia (Nigeria), Fally Ipupa (DRC), Navio (Uganda) na Amani (Kenya). 

Kwenye mradi huo, R. Kelly aliwakutanisha mastaa hao huku yeye akiwa kama mtunzi na mtayarishaji wa wimbo uitwao ‘Hands Across the World’ uliolenga kuonesha umoja wa bara la Afrika kupitia muziki.

Hata hivyo wimbo huo ulifanikiwa kutoka Novemba 2010, licha ya kuwa na ushirikiano wa wasanii wakubwa akiwamo R. Kelly kama mtayarishaji mkuu, haukufanikiwa sana kimauzo wala kupenya kwenye chati nyingi duniani kama ilivyotarajiwa. Lakini ulisaidia kuwapa wasanii wa Afrika akiwamo Alikiba kutambulika zaidi kimataifa kupitia mradi wa One8 Project.

Mbali na kufanya kolabo hiyo lakini pia Kiba alifanikiwa kupata nafasi ya kushoot video na kurekodi sauti ya wimbo huo sambamba na kufanya mazungumzo ya kazi na R. Kelly, ambayo yalimpa maarifa mapya kuhusu nidhamu ya kazi, uandishi wa nyimbo na matumizi ya sauti kwenye muziki wa kimataifa.

Mradi wa ‘One8 Project’ uliishia kuachia kolabo hiyo moja kisha ukasimama kutokana na changamoto za usimamizi ambapo baada ya mwanzilishi wake Kelly kukumbwa na kesi zilizopelekea kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

Mpaka kufika sasa mradi huo hakuna msanii wala kampuni inayoendeleza huku mastaa kama 2Face akiendelea kukuukumbuka kutokana na kumtambulisha kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *