
Mkuu wa jeshi la polisi nchini Tanzania, Camilius Wambura, ametangaza makataa ya watu kutotembea usiku katika jiji la kibiashara la nchi hiyo Dar es Salaam, kufuatia maandamano ya vurugu katika baadhi ya maeneo.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Tangazo la IGP Wambura, limekuja saa chache kupita tangu kufungwa rasmi kwa zoezi la upigaji kura nchi nzima, baadhi ya maeneo kura zikiwa zimeanza kuhesabiwa.
Majira ya asubuhi, polisi kwenye maeneo kadhaa ya jiji la Dar es Salaam, walikabiliana na baadhi ya waandamanaji waliojitokeza barabarani kupinga kile wamesema uchaguzi wa upande mmoja.
Mabomu ya machozi na risasi za mpira zilitumika kujaribu kuwatawanya waandamanaji waliojitokeza, ambao baadhi yao walichoma moto mali na hata kujaruhi baadhi ya askari, hii ni kwa mujibu wa watu walioshuhudia vurugu hizo.
Hii ilikuwa ni mara ya kwanza katika historia ya taifa hilo kwa raia ambao wengi ni vijana kujitokeza barabarani kufuatia wito uliokuwa ukitolewa kupitia mitandao ya kijamii, kilichofanyika kikifananishwa na kile kilichofanyika Kenya na baadae Madagascar.
Hata hivyo katika taarifa ya jeshi la Polisi, haikusema makataa hayo yatadumu hadi lini.
Matokeo rasmi ya uchaguzi huu yanatarajiwa kutangazwa mwishoni mwa juma hili, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kupata ushindi wa kishindo, katika uchaguzi ambao chama kikuu cha upinzani, Chadema hakikushiriki.
Aidha mwenyekiti wake Tundu Lissu, anazuiliwa gerezani akikabiliwa na kesi ya tuhuma za uhaini, madai ambayo wakati huu kesi yake ikiendelea amekana shtaka hilo.