Guterres amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zinaongezeka kwa kasi zaidi kuliko uwezo wa dunia kukabiliana nazo, huku fedha za kukabiliana na athari hizo hazitoshelezi.
“Athari za tabianchi zinaongezeka kwa kasi,” amesema Guterres. “Lakini fedha za kusaidia kukabiliana nazo hazilingani na kasi hiyo, na hivyo kuwaacha watu walio hatarini zaidi wakikabiliwa na kina cha bahari kinachojaa, dhoruba hatari na joto kali lisilovumilika.”
Nchi zinazoendelea zinahitaji fedha mara 12 zaidi
Kwa mujibu wa ripoti hiyo mpya ya Umoja wa Mataifa, mahitaji ya kifedha ya nchi zinazoendelea kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ni mara kumi na mbili zaidi ya kiwango cha fedha wanachopokea kwa sasa.
Guterres amesisitiza kuwa “Hili si pengo la kifedha pekee, ni kushindwa kwa mshikamano wa kimataifa”.
Ameongeza kuwa pengo hilo” Linapimwa kwa nyumba zilizofurika, mazao yaliyoharibika, maendeleo yaliyokwama na maisha yaliyopotea.”
Mabadiliko ya kuelekea nishati safi, kama vile nishati ya jua, yanaongezeka kwa kasi duniani kote.
Wito wa hatua madhubuti katika COP30 nchini Brazil
Akiangazia mkutano ujao wa tabianchi wa Umoja wa Mataifa, COP30, utakaofanyika nchini Brazil, Guterres amewataka viongozi wa dunia kukubaliana kuhusu mpango wa kimataifa wa utekelezaji utakaohakikisha nchi zinazoendelea zinapata rasilimali na uwezo wa kulinda watu wao, kuimarisha uhakika wa chakula na maji, na kujenga uimara katika sekta zote za maendeleo.
Ameyataka mataifa yaliyoendelea kutimiza ahadi zao zilizochelewa za kuongeza mara mbili ufadhili wa miradi ya kujenga mnepo, na watoa huduma za kifedha kutekeleza Ramani ya Njia ya Baku hadi Belém, inayolenga kuchangisha dola trilioni 1.3 kila mwaka ifikapo 2035 huku sehemu ya haki na thabiti ikitengwa kwa ajili ya kujenga mnepo.
“Fedha mpya hazipaswi kuongeza mzigo wa madeni,” alionya.
Sekta binafsi na benki za maendeleo zihusishwe zaidi
Katibu Mkuu pia amezitaka sekta binafsi kuwekeza zaidi katika miradi ya kujenga mnepo na kukabiliana na tabianchi, akisisitiza kwamba faida za mafuta kisukuku zinapaswa kusaidia kurekebisha madhara yaliyosababishwa nayo.
Pia amezitaka benki za maendeleo za kimataifa kuongeza ufadhili nafuu wa kibinafsi na kuelekeza nusu ya fedha zao za tabianchi katika miradi ya kujenga mnepo.
Aidha, amesema fedha za umma za tabianchi lazima ziwe rahisi na za haraka kupatikana, ili ziweze kufikia jamii zilizo mstari wa mbele wa athari za tabianchi wakati na mahali zinapohitajika zaidi.”
Mjumbe wa kijijini wa kamati ya kupunguza hatari ya maafa wakati wa majanga akiwasilisha ujumbe wa onyo la mapema kwa wakazi wa kijiji kilicho kwenye kingo za Mto Licungo katika Mkoa wa Zambezia, Msumbiji.
Tahadhari za mapema kwa wote kufikia 2027
Guterres amesisitiza tena umuhimu wa kutekeleza mpango wa Tahadhari za Mapema kwa Wote ifikapo mwaka 2027, unaolenga kuhakikisha kila mtu duniani analindwa dhidi ya majanga ya tabianchi kupitia taarifa za mapema na tahadhari kwa wakati.
Akihitimisha, Katibu Mkuu akisisitiza kuwa mnepo haupaswi kuonekana kama gharama, bali ni uwekezaji muhimu kwa uhai wa binadamu.
Amesema “Mnepo si gharama ni njia ya kuokoa maisha. Kuziba pengo la mnepo ndiyo njia ya kulinda maisha, kutoa haki ya tabianchi, na kujenga dunia salama na endelevu zaidi. Tusipoteze muda mwingine tena.”