
Katika kile kinachoibua maswali mazito kuhusu usafirishaji wa silaha na ushawishi wa mataifa ya nje katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, ripoti mpya imefichua kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imewasambazia waasi wa RSF silaha na vifaa vya kijeshi vilivyotengenezwa Uingereza.
Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, mifumo ya kulenga shabaha na injini za magari ya kivita kutoka Uingereza imekutwa kwenye medani za mapigano nchini Sudan, hasa katika maeneo ya Khartoum na Omdurman. Vifaa hivyo vinadaiwa kuwa vya kampuni ya Militec yenye makao yake Wales, na viligunduliwa katika kambi zilizokuwa zikimilikiwa na waasi watenda jinai wa RSF.
Ripoti hiyo inarejelea mafaili mawili ya nyaraka yaliyokusanywa na jeshi la Sudan, yenye tarehe za Juni 2024 na Machi 2025, ambayo yamewasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama ushahidi wa moja kwa moja wa msaada wa UAE kwa waasi wa RSF.
Katika wiki za hivi karibuni, RSF ilitwaa udhibiti wa mji wa el-Fasher, eneo la Darfur Kaskazini, ambapo mashirika ya misaada yameripoti mauaji, uvamizi wa hospitali, na hali ya taharuki. Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa waasi wa RSF wametekeleza mauaji ya raia waliokuwa wakijaribu kukimbia, huku kukiwa na dalili za chuki za kikabila dhidi ya jamii ya Wamasalit.
Tangu mwaka 2023, mapigano kati ya jeshi la Sudan na RSF yamesababisha vifo vya makumi ya maelfu na kuwafurusha zaidi ya watu milioni 12. Shirika la Kimataifa la Uokoaji (IRC) limeutaja mgogoro huo kuwa “janga kubwa zaidi la kibinadamu kuwahi kurekodiwa.”
Serikali ya Sudan imeishtumu UAE kwa kuunga mkono kile inachokiita “mauaji ya halaiki” dhidi ya Wamasalit wasio Waarabu katika eneo la Darfur. Mwezi Aprili mwaka huu, Sudan iliwasilisha kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ikidai kuwa UAE ndiyo “inayochochea” mauaji hayo, na kuitaka ilipe fidia kamili kwa waathirika wa vita hivyo.
Kwa mujibu wa mashirika ya haki za binadamu, RSF imehusika na mauaji ya halaiki, ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, na uharibifu wa miundombinu ya kiraia. Umoja wa Mataifa umeendelea kutoa tahadhari kuhusu hatari ya kuenea kwa ukatili huo katika maeneo mengine ya Sudan.
Ripoti hii inazidi kuibua wasiwasi kuhusu jukumu la mataifa ya Kiarabu na ya Magharibi katika migogoro ya Afrika, na kuibua wito wa uwajibikaji wa kimataifa na ukomeshaji wa usambazaji wa silaha kwa makundi yenye rekodi ya ukiukaji wa haki za binadamu.