Serikali ya Madagascar inayoongozwa na jeshi leo imetangaza baraza la mawaziri linalojumuisha idadi kubwa ya mawaziri wa kiraia.

Baadhi ya mawaziri hao ni wakosoaji wakuuu wa rais aliyeondolewa madarakani Andry Rajoelina.

Baraza hilo la mawaziri la Waziri Mkuu Herintsalama Rajaonarivelo, lililotangazwa kupitia televisheni ya taifa ya TVM, linawajumuisha raia 25 na wanajeshi wanne.

Christine Razanamahasoa aliyeondolewa kwenye wadhifa wa uspika wa bunge na chama cha Rajoelina mwaka jana, sasa ameteuliwa kuwa waziri wa mambo ya kigeni.

Mpinzani wa Rajoelina aliyekuwa anaishi uhamishoni Fanirisoa Ernaivo ametajwa kuwa waziri wa sheria.

Uteuzi huo wa baraza la mawaziri ni hatua muhimu katika siasa za Madagascar zilizokumbwa na msukosuko, huku jeshi likishikilia madaraka na kujaribu kuimarisha uchumi na migawanyiko ya kisiasa.

Rais wa zamani wa Madagascar, Andry Rajoelina wiki iliyopita alivuliwa uraia wake baada ya kuikimbia nchi hiyo mapema mwezi huu kufuatia maandamano makubwa yaliyoongozwa na vijana dhidi ya utawala wake.

Wiki za mwisho za kuwepo madarakani Andry Rajoelina ziliathiriwa na maandamano ya maelfu ya wananchi wa Madasgascar waliokuwa wakilalamikia tatizo la umeme, ukosefu wa maji, kupanda gharama za maisha na ufisadi.

Maandamano yaliyoongozwa na vijana yalizuka Septemba 25 kutokana na uhaba mkubwa wa maji na umeme, pamoja na madai ya rushwa, baadaye yaligeuka haraka kuwa wito wa kumtaka aliyekuwa rais wa nchi hiyo Rajoelina ajiuzulu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *