Leo ni siku ambayo Watanzania wenye sifa na waliojiandikisha kwenye Daftari la Mpigakura, wanakwenda kutekeleza jukumu zito la kuwachagua viongozi watakao iyongoza nchi yao kwa miaka mitano ijayo.

Ilikuwa ni safari ya miezi 2 ya kampeni za vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu kumnadi ilani za vyama vyao sambamba na kuomba kura kwa wananchi, iliyoanza Agosti 28, 2025 na kuhitimishwa jana Jumanne Oktoba 28, leo ndiyo siku muhimu.

Nasema ni siku muhimu kwa sababu Watanzania ndiyo wanalisogelea sanduku la kura na wataamua waende na nani kwenye safari hiyo mpya ya miaka mitano ijayo.

Kila chama kimekuwa kikijitahidi kushawishi wananchi kukiamini kama chaguo bora la kuliongoza taifa katika miaka mitano ijayo.

Hata hivyo, tunapaswa kutambua kwamba uchaguzi ni tukio la muda, lakini Tanzania ni ya kudumu. Baada ya kura kupigwa na matokeo kutangazwa, maisha yataendelea na swali kuu la kujiuliza, tutayaendelezaje maisha yetu baada ya uchaguzi huku tukiwa wamoja wenye amani na mshikamano?

Kwa zaidi ya nusu karne tangu tupate uhuru, Tanzania imeendelea kuwa kisiwa cha amani katika bara ambalo nchi zake nyingi hukumbwa na migogoro baada ya uchaguzi.

Hii ni heshima kubwa tuliyopewa na vizazi vilivyotutangulia, hasa kutokana na busara ya viongozi wetu walioweka mbele umoja wa kitaifa kuliko maslahi ya kisiasa.

Leo tunapokamilisha kazi hii kubwa ya uchaguzi mkuu, tunapaswa kuenzi misingi hiyo na kuendeleza urithi huo tulioachiwa na waasisi wa Taifa hili. Tunapaswa kuelewa kuwa ushindi wa chama chochote ni ushindi wa Watanzania na kushindwa ni sehemu ya mchakato wa kidemokrasia.

Kukubali matokeo kwa moyo wa uvumilivu ni ishara ya ukomavu wa kisiasa na heshima kwa sauti ya wengi. Endapo kutakuwa na malalamiko, njia bora ni kufuata taratibu za kisheria, si kuchochea ghasia au vurugu ambazo zinaweza kuvuruga amani tuliyoijenga kwa muda mrefu. Baada ya uchaguzi ni kawaida kuona hisia kali, maneno ya majivuno au ya kejeli yakitawala mitandaoni na kwenye majukwaa ya kijamii. Huu ni wakati muhimu wa kujizuia na kuonyesha ukomavu wa kisiasa. Tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa sababu ya kuvunja undugu, marafiki au majirani. Chama utakachokipigia kura hakibadilishi ukweli kwamba sote ni Watanzania tunaoshiriki uchungu, furaha na matumaini ya nchi moja. Tuchukue muda huu kupongezana, si kubezana; kujenga, si kubomoa; kusamehe, si kulipiza.

Uchaguzi unapomalizika, jukumu letu kubwa linabaki kuwa ni kuijenga nchi. Serikali mpya itakayoundwa, iwe ni ile iliyokuwa madarakani au itakayoshika usukani kwa mara ya kwanza, inahitaji ushirikiano wa wananchi wote.

Hakuna maendeleo yatakayopatikana endapo tutakubali kugawanywa kisa tu, uchguzi na matokeo yake.

Tunapaswa kukumbuka kuwa kila mmoja wetu analo jukumu katika kuliendeleza Taifa hili kwa nyanja tofauti zikiwamo za uzalishaji, elimu, afya, kilimo, biashara na huduma za kijamii. Tanzania haiwezi kusonga mbele kama tutabaki kupoteza muda katika mijadala ya chuki na lawama zisizoisha.

Viongozi wa kisiasa wanayo nafasi kubwa ya kuamua mustakabali wa nchi baada ya uchaguzi. Maneno yao yana nguvu ya kujenga au kubomoa. Wakati huu ni muhimu kwa viongozi wote, wawe wa chama tawala au wa upinzani, kuwa mfano wa hekima na busara. Ni wakati wa wao kutoa kauli za kuleta utulivu na maridhiano, si za kuamsha hasira au kuchochea mgawanyiko. Uongozi wa kweli ni ule unaoweka mbele maslahi ya Taifa kuliko ya chama au mtu binafsi. Vyombo vya habari pia vina wajibu mkubwa wa kutumia kalamu zao kuhimiza amani, umoja na maendeleo badala ya kuendeleza mijadala ya chuki au fitina baada ya uchaguzi. Uandishi wenye weledi ni ule unaotoa taarifa sahihi, unaoelimisha wananchi na kuwasaidia kuelewa hali halisi bila kupotoshwa.

Waandishi wa habari wanapaswa kutambua kuwa kila neno wanaloandika linaweza kuleta matumaini au kuchochea taharuki.  Mitandao ya kijamii nayo ni silaha yenye pande mbili. Inaweza kujenga maelewano au kusababisha mgawanyiko mkubwa.

Watumiaji wake wanapaswa kutambua kuwa uzalendo hauishii tu kwenye kupiga kura, bali pia kwenye namna tunavyotumia sauti zetu baada ya uchaguzi. Tuandike maneno ya kutuliza, kuhamasisha na kuunga mkono juhudi za kujenga taifa. Tukiendelea kushindana kwa hoja na heshima, tutakuwa tumedhihirisha ukomavu wa kidemokrasia.

Zaidi ya yote, ni muhimu kuendelea kudumisha maadili ya kitaifa yaliyotufanya tuwe na amani kwa muda mrefu.  Heshima, utu, upendo na umoja ni nguzo kuu zinazotuweka pamoja. Wazazi, viongozi wa dini, walimu na wazee wa mila wanapaswa kuwa mstari wa mbele kufundisha vijana thamani ya kuipenda nchi yao. Kura ni sauti ya kuchagua mwelekeo wa maendeleo, si sababu ya kutugawa.

Lilian Timbuka ni Mhariri na Mkuu wa Dawati la Uchaguzi – Mwananchi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *