
Ubalozi wa Marekani nchini Mali umewataka raia wa Marekani kuondoka mara moja wakati huu mashambulio kutoka kwa wanajihadi wanaopambana na serikali inayoongozwa na jeshi la nchi hiyo yakiongezeka kila siku hasa kwenye usafirishaji wa mafuta.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Tangu mwanzo wa Septemba mwaka huu , wapiganaji wanaohusishwa na Al-Qaeda wamelenga meli za mafuta, hasa zile zinazotoka Senegal na Ivory Coast, ambapo bidhaa nyingi zinazoagizwa kutoka Mali hupitia.
Wanajihadi hao kutoka Kundi linaunga nga Mkono Uislamu na Waislamu, linalojulikana kama JNIM, hata hivyo limeonekana kutaka kuutenga mji mkuu Bamako kwa kuongeza mashambulizi hasa kwenye barabara zinazouzunguka mji huo .
Ubalozi wa Marekani ulisema katika taarifa kwenye tovuti yake kwamba Raia wa Marekani “wanapaswa kuondoka mara moja kwa kutumia usafiri wa anga za kibiashara”, wakati huu hali ya usalama wa Bamako ikionekana kudorora
Licha ya kusindikizwa na kupewa ulinzi na jeshi la Mali , meli za mafuta zimekuwa na mafanikio machache kufika Bamako,huku mengi ya malori hayo yakichomwa moto , madereva na wanajeshi wakiuawa au kutekwa nyara katika mashambulizi ya kuvizia ya wanajihadi.
Mali imekuwa ikipambana na utovu wa usalama kwa zaidi ya muongo mmoja unaochochewa na ghasia za wanajihadi wanaohusishwa na Al-Qaeda na kundi la Islamic State, pamoja na wahalifu na magenge mengine.
Nchi hiyo ambayo pia ilipitia mapinduzi mnamo 2020 na 2021 na inayoongozwa na utawala wa kijeshi , imejitahidi kukabiliana na vikundi vyenye silaha bila mafanikio.