Matukio chanya yametokea katika wiki za hivi karibuni katika suala la kuongeza uhusiano wa kibiashara na mawasiliano kati ya Iran na Pakistan.
Balozi wa Pakistan mjini Tehran, Muhammad Mudassir Tipu alitangaza tarehe 19 Oktoba kwamba, agizo jipya la kiutendaji la serikali ya nchi hiyo lilitolewa baada ya mchakato mrefu na kuzingatiwa wasiwasi wa jumuiya za wafanyabiashara wa Iran na Pakistan, kwa lengo la kupanua biashara ya pamoja ya mabadilishano na Jamhuri ya Kiislamu.
Tipu aliandika ujumbe kwenye akaunti yake rasmi kwenye mtandao wa kijamii wa X: “Pakistani imetoa Amri mpya ya Utendaji (SRO) ya kukuza biashara ya mabadilishano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Balozi wa Pakistan nchini Iran alieleza matumaini yake kwamba amri hii itaimarisha kwa kiasi kikubwa kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili jirani.”
Tarehe 2 Oktoba, Wizara ya Fedha ya Pakistan iliidhinisha rasimu iliyowasilishwa na Wizara ya Biashara ya nchi hiyo kwa ajili ya kurekebisha makubaliano ya biashara ya baina ya pande mbili na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na siku chache baadaye, baraza la mawaziri la serikali likiongozwa na Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif lilikubali uamuzi huo wa Kamati ya Uratibu wa Kiuchumi.
Katika hatua nyingine inayolenga kuongeza uhusiano kati ya Iran na Pakistan, Waziri wa Barabara na Maendeleo ya Miji wa Iran Farzana Sadiq na Waziri wa Usafirishaji wa Meli wa Shirikisho la Pakistan Muhammad Junaid Anwar Chaudhry walikutana mjini Islamabad Oktoba 24 kujadili njia za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kupitia usafiri wa baharini.

Huku zikitilia mkazo maendeleo ya miundombinu ya bandari na kuboresha njia za usafirishaji, pande hizo zilipendekeza kuzindua njia ya moja kwa moja ya meli kati ya nchi hizo mbili ili kuimarisha biashara, utalii na mabadilishano ya kikanda.
Maafisa hao wawili wa Iran na Pakistan pia walisisitiza umuhimu wa kuimarisha mawasiliano ya kikanda ili kukuza biashara, kuvutia uwekezaji na kupanua mashirikiano ya kiraia. Kadhalika walijadili mipango mbalimbali ya kuwezesha biashara ya baharini, kuendeleza miundombinu ya bandari, na kuboresha njia za usafirishaji zinazounganisha nchi hizo mbili kupitia kanali za bahari, ardhi na reli.
Waziri wa Usafiri wa Meli wa Pakistan alipendekeza kuanzishwa kwa njia ya meli ya moja kwa moja kati ya Pakistan na Iran, akisisitiza kwamba huduma hii inaweza kuwa njia mbadala ya gharama nafuu na yenye ufanisi ili kukuza utalii na shughuli za kibiashara.
Ameongeza kuwa: “Kuzinduliwa kwa njia hii ya meli sio tu kutaongeza biashara baina ya nchi mbili, bali pia kutatoa fursa ya usafiri wa kiuchumi kwa mazuwwar (wafanyaziara) wanaozuru Iran na Iraq.”
Waziri wa Barabara wa Iran, alipokuwa akikaribisha pendekezo la upande wa Pakistan, alizitaja bandari za nchi hizo mbili kuwa rasilimali muhimu ya kiuchumi ambayo inaweza kuwa lango la biashara ya kikanda.
Sambamba na kuashiria kwamba, kuboreshwa mawasiliano ya bahari, usafiri na uchukuzi kunaweza kufungua upeo mpya kwa ajili ya biashara ya kieneo na bandari za Iran na Pakistan kuwa na nafasi muhimu katika hilo alisisitiza juu ya pande mbili kujifunga na kuheshimu ushirikiano huo kwa minajili ya kuongeza ushirikiano wa bandari na kuchuunguza njia mpya za kibiashara katika bahari ya Arabu na Ghuba ya Uajemi.
Kiujumla, kuongezeka kwa mahusiano ya kibiashara na mawasiliano kati ya Iran na Pakistan kunaweza kuleta manufaa makubwa kwa nchi zote mbili. Nchi hizi mbili jirani zenye mfanano wa kitamaduni, kidini na kihistoria, zina uwezo mkubwa wa ushirikiano wa kiuchumi na mawasiliano, ambao ukitumiwa ipasavyo unaweza kuchangia maendeleo endelevu ya eneo hili.
Kwa mtazamo wa kiuchumi, Iran, pamoja na rasilimali zake nyingi za nishati na eneo la kimkakati katika kanda, inaweza kuwa msambazaji wa kuaminika wa mahitaji ya nishati ya Pakistan. Kinyume chake pia, Pakistan, ikiwa na idadi kijana ya watu na soko kubwa la watumiaji, inatoa fursa nzuri ya kusafirisha bidhaa za Iran.

Kustawishwa miundombinu ya uchukuzi, ikijumuisha reli na barabara za mpakani, kunaweza kuwezesha biashara baina ya nchi na kupunguza gharama za miamala.
Katika nyanja za kivitendo, kitamaduni na vyombo vya habari, kupanuliwa ushirikiano wa kisayansi, kitamaduni na vyombo vya habari kunaweza kuimarisha uhusiano kati ya watu na kuongeza maelewano kati ya mataifa hayo mawili. Mabadilishano ya wanafunzi, kufanya maonyesho ya pamoja, na ushirikiano wa kitaaluma ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuimarisha mafungamano ya kibinadamu.
Pia, usalama na ushirikiano wa kimipaka kati ya Iran na Pakistan unaweza kusaidia kupunguza vitisho vya pamoja kama vile magendo, ugaidi na misimamo ya kufurutu mpaka. Kuanzisha mifumo ya pamoja ya usimamizi wa mpaka na ubadilishanaji wa taarifa za usalama kutakuwa na jukumu muhimu katika utulivu wa kikanda.
Kiujumla tunaweza kusema kuwa, kuongezeka uhusiano wa kibiashara na mawasiliano kati ya Iran na Pakistan sio tu kwamba kuna manufaa ya kiuchumi na kiutamaduni kwa nchi hizo mbili, bali kunaweza pia kupelekea kuimarisha amani, uthabiti, utuulivu na ushirikiano wa kieneo Kusini Magharibi mwa Asia.