Ripoti rasmi inaonyesha kuweko ongezeko la majaribio ya kujitoa mhanga miongoni mwa wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel katika kipindi cha miezi 18 iliyopita.

Ripoti hiyo, iliyotayarishwa na Kituo cha Utafiti na Habari cha Bunge la Israel Knesset, inaonyesha kwamba majaribio 279 ya kujiua yalirekodiwa kuanzia Januari 2024 hadi Julai 2025.

Ripoti hiyo ya inaonyesha kuwa wanajeshi 124 wa Israel walijiua kuanzia 2017 hadi 2025, ambapo 68% walikuwa askari wa kazi, 21% walikuwa askari wa akiba, na 11% walikuwa wanajeshi rasmi wa Israel.

Ripoti hiyo pia inaashiria ongezeko kubwa la watu wanaojiua miongoni mwa askari wa akiba tangu 2023, huku sehemu ya kundi hili ya jumla ya watu waliojiua ikiongezeka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni.

Hapo awali gazeti la Kizayuni la “The Times of Israel” liliripoti kuwa, matukio mengi ya kujiua ya hivi karibuni ya askari wa jeshi la utawala huo ghasibu yanahusiana na kuwepo kwao kwa muda mrefu katika maeneo ya vita na kushuhudia matukio ya kutisha na kupoteza wenzao katika vita.

Pamoja na ripoti hiyo, lakini hadi sasa jeshi la utawala wa Kizayuni limekataa kutoa takwimu za idadi rasmi ya askari wake waliojiua, licha ya kuahidi mara kadhaa kuwa litafanya hivyo.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, maombi ya Wazayuni ya kutaka huduma za msaada wa kisaikolojia kutokana na vita na Iran yameongezeka kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa tangu kuanza kwa vita kati ya utawala huo na Iran, sambamba na dalili za kuongezeka matatizo ya ndani katika nyanja ya afya ya akili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *