Rais Donald Trump wa Marekani ameamuru kuanzishwa tena majaribio ya silaha za nyuklia za nchi hiyo.
Trump ametangaza katika ujumbe wake kwenye akaunti ya mitandao ya kijamii, Truth Social, kwamba ameiagiza Wizara ya Vita kuanza tena majaribio ya silaha za nyuklia. Ameeleza kwamba: “Kutokana na programu za majaribio ya nyuklia za nchi zingine, nimeiagiza Wizara ya Vita kuanza kujaribu silaha zetu za nyuklia kama wao wanavyofanya, na hili litaanza mara moja.”
Donald Trump amedai kwamba uamuzi huo umechukiliwa kutokana na mipango ya majaribio ya nyuklia ya nchi nyingine na kwamba mchakato wa kuutekeleza utaanza mara moja. Kwa hivyo, Trump ameamuru Wizara ya Vita kuanza tena majaribio ya nyuklia sambamba na hatua zilizochukuliwa na Russia na Uchina. Amedai kwamba Marekani ina idadi kubwa zaidi ya silaha za nyuklia na kwamba agizo hilo ni sehemu ya uboreshaji na usasishaji wa silaha za nyuklia za nchi hiyo. Amesema, uamuzi huu umechukuliwa kwa kulazimishwa na unalenga kudumisha “mlingano wa nguvu” dhidi ya vitisho vinavyoongezeka duniani.

Uamuzi huo unakuja huku Russia ikitangaza hivi karibuni kwamba imefanya kwa mafanikio majaribio ya torpedo ya nyuklia, na China imepanua programu zake za silaha za nyuklia. Trump amesisitiza kwamba: “Russia iko katika nafasi ya pili, na China iko katika nafasi ya tatu kwa mbali, lakini itatufikia ndani ya miaka mitano ijayo.”
Agizo la Rais wa Marekani la kuanza tena majaribio ya silaha za nyuklia nchini humo limezidisha mvutano wa kimataifa na kuimarisha uwezekano wa mashindano mapya ya silaha za nyuklia. Uamuzi huo umepokewa kwa hisia za wasiwasi kutoka taasisi za kimataifa na nchi mbalimbali. Wachambuzi wengi wanaamini kwamba, hatua hii inaweza kudhoofisha makubaliano ya kimataifa kama vile Mkataba Kamili wa Kupiga Marufuku Majaribio ya Nyuklia (CTBT) na kuzidisha hali ya kutoaminiana miongoni mwa mataifa makubwa duniani. Vilevile, agizo hilo linaweza kuwa kisingizio kwa nchi zingine kustawisha zaidi miradi yao za silaha za nyuklia.
Jambo la kutiliwa maanani ni kwamba, hata maafisa wakuu wa usalama wa Marekani wamekiri ukweli huu. Hivi karibuni, Mkurugenzi wa Ujasusi wa Kitaifa wa Marekani, Tulsi Gabbard alionya kuhusu hatari za vita vya nyuklia akisisitiza kwamba: “Leo, dunia iko karibu zaidi ya ukingo wa maangamizi ya nyuklia.”
Kwa ujumla, kuanza tena kwa majaribio ya silaha za nyuklia huko Marekani kunaweza kuwa na matokeo mabaya sana ikiwa ni pamoja na kuongezeka mvutano kati ya mataifa yenye nguvu za silaha za nyuklia kama vile Russia, Uchina na Marekani, kudhoofika mikataba ya kudhibiti silaha, kuongeza uwezekano wa nchi kujiondoa katika mikataba ya kimataifa na kuhamasisha nchi za kikanda kuendeleza programu zao za silaha za nyuklia, na vilevile kuongezeka hatari ya migogoro ya kijeshi kwa kutumia silaha za maangamizi.
Uamuzi huu wa Trump ni kinyume na sera ya muda mrefu ya Marekani. Jaribio la mwisho la silaha za nyuklia la Marekani lilifanyika Septemba 23, 1992, muda mfupi kabla ya rais mrepublican wa wakati huo, George W. Bush kusimamisha majaribio hayo mwishoni mwa Vita Baridi. Kwa mujibu wa taarifa ya Maabara ya Kitaifa ya Los Alamos, jaribio la mwisho la silaha za nyuklia la Marekani, lililopewa jina la “Divider,” lilikuwa jaribio la 1054 la nyuklia nchini humo na lilifanyika katika kituo cha chini ya ardhi huko Nevada. Kituo hicho kinaweza kutumika tena kwa majaribio ya silaha za nyuklia.

Kutokana na uamuzi wa sasa wa Trump, uwezekano wa kurudi kwenye enzi ya mashindano ya silaha za nyuklia umeongezeka. Mataifa yenye silaha za nyuklia, hasa Russia na China, yanaweza kutumia fursa ya Marekani kuanza tena majaribio ya nyuklia kuchukua hatua kama hizo, na hivyo kufungua njia kwa Ufaransa na Uingereza kuanza tena majaribio ya silaha za nyuklia.
Hivyo, agizo la Trump la kuanza tena majaribio ya silaha za nyuklia nchini Marekani mbali na kutishia usalama wa dunia, lakini pia linaweza kuchochea mashindano ya silaha za nyuklia. Katika hali kama hiyo, kunaonekana umuhimu mkubwa zaidi kwa jamii ya kimataifa kuwa na nafasi kubwa katika kudhibiti mgogoro na kuzuia kuenea kwa silaha za maangamizi makubwa. Ni kupitia ushirikiano, uwazi na diplomasia pekee ndipo tunaweza kuzuia kurudi kwenye enzi za giza za Vita Baridi.