Leo ni Ijumaa tarehe 09 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1447 Hijria sawa na Oktoba 31 mwaka 2025 Milaadia.
Tarehe 9 Jamadil Awwal mwaka 786 Hijria, aliuawa shahidi faqihi na mtaalamu mkubwa wa Hadithi, Muhammad bin Jamaluddin Makki Amili, mashuhuri kwa jina la “Shahidi wa Kwanza.”
Alizaliwa mwaka 734 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Jabal Amil nchini Lebanon. Alijifunza elimu mbalimbali kutoka kwa walimu wakubwa wa zama zake kama vile Allama Hilli. Mbali na elimu ya dini, Muhammad bin Jamaluddin pia alikuwa hodari katika taaluma za mashairi na fasihi.
Katika miaka 52 ya umri wake uliojaa baraka, Shahidi wa Kwanza aliandika vitabu vingi, ikiwa ni pamoja na “Albaqiyatus-Swalihat” na “al Lumuatu Dimashqiyya.” Aliuawa na wapinzani wenye taasubi katika siku kama ya leo.

Katika siku kama ya leo miaka 467 iliyopita alizaliwa katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran Ṣadruddin Muḥammad bin Ibrahim al-Shirazi maarufu kwa jina la Ṣadrul Muta’allihīn au Mulla Sadra, mwanafalsafa na arif mkubwa wa Kiislamu.
Awali alielekea katika mji wa Qazwin uliokuwa katika zama hizo mji mkuu wa utawala wa Safavi na kuhudhuria darsa na masomo ya walimu wakubwa kama Sheikh Bahai. Alisoma Fikihi, Usul, hadithi na hisabati kwa Sheikh Bahai na kusoma mantiki, falsafa na Irfan kwa Mirdamad. Baada ya Isfahan kufanywa mji mkuu, Mulla Sadra naye alihamia katika mji huo na kuanza kufundisha.
Hata hivyo kutokana na mitazamo yake kupingana na maulama kadhaa, Mulla Sadra alilazimika kuuhama mji huo na kuanza kuishi katika kijiji cha karibu na mji wa Qum. Baada ya muda alianza tena kujishughulisha na kazi ya kufundisha na kualifu vitabu.
Al Mabdau Wal-Maad, Zadul Musafir na Mutashaabihaat al-Qur’an ni baadhi tu ya vitabu vya Ṣadrul-Muta’allihīn.

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, yaani tarehe 9 Aban 1304 Hijria Shamsia, Bunge la Ushauri la Taifa la Iran lilichukua uamuzi wa kumuuzulu Ahmad Shah, mfalme wa mwisho wa silsila ya Qajar na kutangaza kuufuta kikamilifu utawala wa kizazi hicho nchini Iran kilichobaki madarakani kwa kipindi cha miaka 135.
Baada ya kuondoshwa utawala wa silsila ya Qajar, Uingereza ilifanya njama za kuingilia kati na kuuweka madarakani utawala wa muda nchini ulioongozwa na Reza Khan. Reza Khan alijitangaza kuwa mfalme na kuanzisha silsila ya utawala wa Kipahlavi. Utawala huo wa Kipahlavi uliandaa mazingira ya kuporwa zaidi utajiri wa taifa na kukandamizwa wananchi wa Iran kulikofanywa na madola ya Uingereza na Marekani.

Tarehe 31 Oktoba 1984 yaani siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, aliuawa Bi. Indira Gandhi, Waziri Mkuu wa wakati huo wa India.
Mauaji hayo yalifanywa na walinzi wawili wa kiongozi huyo ambao walikuwa Masingasinga. Masingasinga hao walifanya mauaji hayo baada ya Gandhi kutoa amri ya kushambuliwa hekalu la dhahabu lililoko katika jimbo la Punjab, ambalo lilihesabiwa na masingasinga kuwa ni eneo takatifu.
Masingasinga ambao wanaunda asilimia mbili ya watu wa India na wengi wao wanaishi katika jimbo la Punjab, walikusanya silaha zao kwenye hekalu hilo kwa shabaha ya kufanya uasi na kutaka kujitenga jimbo hilo.

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio nambari 540 baada ya utawala wa Baathi wa Iraq kushambulia meli za kibiashara katika Ghuba ya Uajemi.
Azimio hilo lilitolewa kufuatia mashambulizi ya utawala wa Iraq dhidi ya meli za kibiashara katika kipindi cha vita vyake vya kichokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hujuma ambazo zilikuwa na lengo la kuchafua usalama wa eneo hilo. Azimio hilo lilisisitiza haki ya meli zote za kibiashara kufanya safari kwa uhuru katika maji ya kimataifa na lilizitaka nchi zote kuheshimu suala hilo.
Azimio nambari 540 la Baraza la Usalama pia lilizitaka pande mbili hasimu kukomesha mapigano katika Ghuba ya Uajemi na kuheshimu ardhi ya nchi za eneo hilo. Inafaa kuashiria kuwa, azimio hilo lilitolewa huku utawala wa Saddam Hussein ukizidisha mashambulizi yake dhidi ya meli za mafuta za Iran.

Na katika siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, aliaga dunia Federico Fellini mtengenezaji filamu maarufu wa Kiitalia. Fellini ni miongoni mwa watengenezaji na waongozaji filamu wakubwa wa karne ya ishirini. Fellini alianza kazi ya kuandika filamu tangu mwaka 1938 na baadaye akajiingiza katika utengenezaji filamu.
Baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia mwaka 1945, Federico Fellini akiwa msaidizi wa mtengeneza filamu aliyejulikana kwa jina la Roberto Rossellini walitengeneza filamu iliyojulikana kwa jina la “Rome Open City”. Mwaka 1993, yaani miezi sita kabla ya kifo chake, Fellini alitunukizwa tuzo ya Oscar kutokana na kazi zake za thamani katika ulimwengu wa filamu.

