
Rais Erdogan alitoa hotuba pana katika Jukwaa la TRT World 2025 siku ya Ijumaa, akilaani mauaji ya halaiki yanayofanywa na Israel huko Gaza na kukosoa kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kusimamia haki, amani, na maadili.
Erdogan amehoji misimamo inayotetea Israel, akisema: “Israel ina silaha za nyuklia na uwezo wa kushambulia Gaza, popote na wakati wowote inavyotaka; inawezaji kuwa haina hatia?”
Erdogan alikosoa Israel kwa kutumia njaa kama silaha, hasa kuwalenga watoto wakati wa mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu kuwahi kutokea.
“Israel inatumia njaa kama silaha mbaya, hasa dhidi ya watoto,” alisema.
“Huko Gaza, hakuna hata jengo moja lililobakia. Shule, makanisa, misikiti, na hospitali zote zimeharibiwa kwa mabomu. Wanasema, ‘Israel haina hatia.’ Kivipi haina hatia?”
Erdogan pia alikosoa “mfumo wa propaganda ya Israel uliyojengwa kwa misingi ya uongo”, akifichua madhara yake kwa waandishi wa habari.
“Wakiwa dhidi ya mashine ya propaganda ya Israel, waandishi 270 wa habari waliotaka kufichua ukweli wa eneo hilo na kuonyesha uongo wa Tel Aviv wameuawa,” alisema, akisisitiza jukumu la kimaadili la vyombo vya habari kusimama na haki.
Kiongozi wa Uturuki alikosoa taasisi za kimataifa zinazohusika na kudumisha amani na utulivu, zimefumbia macho na kushindwa kuzuia mauaji na halaiki.
“Wale waliowajibika kulinda amani ya dunia wamekosa kuzuia mauaji ya halaiki, na kuokoa maisha ya watoto,” Erdogan alisema.