Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ndizo tawala zinazochukiwa zaidi duniani.

Hujjatul-Islam Mohammad Javad Haj Ali Akbari amesema hayo leo mbele ya hadhara ya waumini waliohudhuria ibada ya Swala ya Ijumaa katika Chuo Kikuu cha Tehran na kubainisha kwamba, mtazamo wa Marekani kuhusu Iran sio makhsusi kwa nchi yetu tu na akakumbusha kuwa, Marekani imechukua mtazamo huu kuhusiana nchi zote duniani, jambo ambalo ni dalili ya kujiona na ujinga wake.

Aidha amesema, Donald Trump Rais wa Marekani anazungumza kana kwamba yeye ndiye bwana wa ulimwengu. Hii ni katika hali ambayo, Marekani na mbwa wake utawala wa Kizayuni, ndio tawala zinazochukiwa zaidi baina ya wananchi na mataifa ya dunia.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya wiki hii mjini Tehran ameongeza kuwa: “Moja ya hatua nzuri zaidi ambazo taifa la Iran lilichukua na ambayo ilifanywa na vijana wake wastahiki ni kuliteka pango la kijasusi (uliokuwa ubalozi wa Marekani mjini Tehran) ambayo Imam Khomeini aliitaja kuwa ni zaidi ya mapinduzi ya kwanza na kuondoa changamoto nyingi za taifa la Iran.”

Hujjatul-Islam Mohammad Javad Haj Ali Akbari ameashiria nafasi ya taifa la Iran katika kukabiliana na ubeberu wa dunia na kusisitiza kuwa, utambulisho huru, unaokua na wenye nguvu wa Iran uliundwa na mafundisho ya Kiislamu na Mapinduzi ya Kiislamu na unaendelea kwa kasi.

Kadhalika amesema “Tunakabiliwa na utambulisho mbaya na ubeberu wa kimataifa ambapo watawala wa Marekani wako tayari kutoa muhanga heshima na maisha ya watu wa dunia kwa ajili ya tamaa na maslahi yao binafsi. Hata hivyo, taifa la Iran likifuata mafunzo na njia ya Imamu Hussein (as) katu halitakubali kudhalilishwa na kamwe halitauza izza, heshima na mamlaka yake ya kujitawala.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *