
Marekani imetangaza siku ya Alhamisi, Oktoba 30, kuanza tena majaribio yake ya silaha za nyuklia, jambo ambalo haikuwa imelifanya tangu mwaka 1992. Tangazo hilo linakuja huku Urusi hivi karibuni ikipata mafanikio katika uwanja wa silaha za nyuklia. Nchi hizi zenye nguvu duniani zinazojifaharisha kwa kupata silaha za nyuklia zinapimana nguvu na kutia wasiwasi Umoja wa Mataifa.
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Hakubainisha tarehe, eneo, au asili ya majaribio haya ya nyuklia. Donald Trump alisema tu kwenye mtandao wake wa Truth Social kwamba “mchakato huu unaanza mara moja.” Hili linaonekana kuwa haliwezekani, kutokana na kubana matumizi kwa serikali nchini Marekani. Hata hivyo, kilicho hakika ni kwamba Rais wa Marekani Donald Trump anataka kuishawishi China, taifa la tatu lenye nguvu za nyuklia duniani; alitoa tangazo lake kabla tu ya kukutana na Xi Jinping nchini Korea Kusini.
Kwa Makamu wa Rais J.D. Vance, majaribio zaidi ya silaha za nyuklia ni muhimu kwa ajili ya utendaji kazi mzuri wa silaha za nyuklia za Marekani. “Tuna silaha kubwa, bila shaka. Urusi ina silaha kubwa za nyuklia. China ina silaha kubwa za nyuklia. Wakati mwingine unahitaji kuzijaribu ili kuhakikisha zinafanya kazi na zinafanya kazi vizuri,” aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House. “Ili kuwa wazi: tunajua zinafanya kazi vizuri, lakini lazima ufuatilie hilo baada ya muda,” alibainisha.
Tangazo la rais wa Marekani pia linakusudiwa kama jibu kwa Vladimir Putin, ambaye amejivunia maendeleo ya siku za hivi karibuni katika uwanja wa silaha za nyuklia. Siku ya Jumapili, Oktoba 26, rais wa Urusi alisherehekea jaribio la mwisho la kombora la Cruz. Na Jumatano, Oktoba 29, alisherehekea jaribio la mafanikio la manowari isiyo na nahodha yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia.
Hata hivyo, Kremlin ilituliza nyoyo viongozi wa dunia siku ya Alhamisi, muda mfupi baada ya ujumbe wa Donald Trump. Kulingana na msemaji wa serikali ya Urusi Dmitry Peskov, majaribio yaliyofanywa Oktoba 26 na 29 hayawezi kuelezewa kama “majaribio ya nyuklia.” “Nchi zote zinafanya kazi katika kukuza ulinzi wao,” lakini majaribio yaliyofanywa na Urusi katika siku za hivi karibuni “hayafanyi kuwa jaribio la nyuklia,” alisema.
Umoja wa Mataifa unapinga majaribio ya nyuklia na una wasiwasi kuhusu “kuongezeka kwa matokeo mabaya”
Iwe Washington au Moscow, taarifa hizo hazina uwazi. Na hizi kimsingi ni za kejeli, kulingana na Jenerali Dominique Trinquand, mkuu wa zamani wa ujumbe wa kijeshi wa Ufaransa kwa Umoja wa Mataifa. “Ni, kwa kutumia neno chafu, mzozo wa madaraka kati ya Bw. Putin na Bw. Trump. Rais wa Urusi Vladimir Putin anatoa matamko kuhusu silaha mpya, za kipekee ambazo Urusi pekee inazo; hii ni propaganda dhahiri – hata kama labda ni kweli – kwa raai wa Urusi. Na ni faida gani, Trump anajibu, kama kawaida, kwamba yeye ndiye mwenye nguvu zaidi,” Jenerali Dominique Trinquand ameiambia RFI.
Donald Trump alitaja “nchi zingine” zinazoendesha programu za majaribio. Labda alikuwa akifikiria Ufaransa? Toleo jipya la kombora la nyuklia la Ufaransa baharini, kwa kweli, lilianza kutumika wiki iliyopita. Lakini rais wa Marekani anasisitiza kwamba lengo lake si kufufua mbio za nyuklia. Hata anadai kutaka kinyume chake.
Farhan Haq, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amebainisha kwamba majaribio ya nyuklia “hayapaswi kamwe kuruhusiwa, kwa hali yoyote ile.” “Hatari za sasa za nyuklia tayari ziko juu sana, na hatua yoyote ambayo inaweza kusababisha hesabu isiyo sahihi au kuongezeka kwa matokeo mabaya lazima iepukwe,” amesema.
Hata hivyo, Dominique Trinquand hakubaliano na matamko ya mataifa yenye nguvu za nyuklia na kusisitiza kanuni ya kuzuia nyuklia, ambayo imezuia matumizi yoyote ya silaha za nyuklia kwa miaka 80 iliyopita: “Silaha za nyuklia hazijatumika tangu mwaka 1945. Na zilitumika wakati huo kwa sababu Marekani pekee ndio iliyokuwa nazo. Leo, hakuna mtu ambaye angehatarisha kutumia silaha za nyuklia, akijua kwamba kulipiza kisasi kwa nyuklia kunaweza kufuata mara moja.”
