Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo vyote dhidi ya Cuba bila masharti yoyote.

Amir Saeed Iravani, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa, siku ya Jumatano alihutubia kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba, akisisitiza kuwa mzingiro huo unapaswa kusitishwa mara moja bila masharti yoyote.

Alisema kuwa kuondoa hatua hizo si tu kutaleta nafuu ya dharura kwa wananchi wa Cuba, bali pia kutatoa ujumbe wa wazi na thabiti kwa dunia kwamba zama za kulazimisha, kutawala kwa mabavu na dhulma za kiuchumi zinapaswa kufikia kikomo.

Akiashiria vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Cuba, Iravani alisema: “Hakuna shaka kuwa vikwazo vya upande mmoja ni vitendo visivyo halali vinavyochochewa na kiburi na sera za upande mmoja, ambavyo vinahatarisha misingi ya ushirikiano wa kimataifa, vinavuruga utulivu wa mfumo wa dunia na kudhoofisha roho halisi ya Katiba ya Umoja wa Mataifa.”

Iravani alisisitiza kuwa kuendelea kwa vikwazo na mzingiro wa upande mmoja na usio wa kibinadamu dhidi ya Cuba, ambavyo vimekuwepo kwa zaidi ya miaka sitini kwa kisingizio cha kuendeleza demokrasia, ni mfano wa wazi wa hatua za kulazimisha dhidi ya taifa huru lenye mamlaka kamili, ambazo kwa mfumo wa kudumu zimepunguza haki na ustawi wa watu wa Cuba.

Aliongeza kuwa Marekani, kwa kuendeleza sera zake za upande mmoja na za mabavu dhidi ya mataifa huru, inaendelea kupuuza kwa makusudi wito wa pamoja na wa wazi wa jumuiya ya kimataifa wa kusitisha uhasama wake dhidi ya Cuba ambao umeendelea kwa zaidi ya miongo sita. Iran imesisitiza tena msimamo wake wa kupinga vikwazo vyovyote vya kiuchumi, kibiashara na kifedha dhidi ya mataifa yenye mamlaka kamili, ikiwemo Cuba.

Jumuiya ya kimataifa kwa kauli moja, kupitia kupitishwa kwa maazimio ya mara kwa mara katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, imekataa kuendelea kwa vikwazo dhidi ya Cuba na kuitaka Marekani kurekebisha sera zake zilizoshindwa na kuondoa mzingiro huo mara moja bila masharti yoyote.

Kwa zaidi ya miaka sitini, Marekani imeiwekea Cuba vikwazo vikali kwa kisingizio kisicho na msingi. Vikwazo vya kwanza vya kiuchumi vya Washington dhidi ya Havana vilianza Februari 1962 kwa amri ya Rais wa wakati huo John F. Kennedy.

Rais wa Cuba, Miguel Díaz-Canel, aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter miaka michache iliyopita, sambamba na maandamano ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya Cuba dhidi ya vikwazo vya kiuchumi vya Marekani, akisema: “Tumepitia miaka 60 ya mapambano na hatujachoka kudai kusitishwa sera hii ya kikatili na iliyopitwa na wakati.”

Amir Saeed Iravani, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa

Serikali ya Havana inaiona Marekani kama chanzo cha shinikizo la kiuchumi linalolenga kuathiri uchumi wa Cuba na kuchochea hali ya kutoridhika ndani ya nchi. Cuba imewasilisha suala hili mara kadhaa katika Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, Cuba imeendelea kustahimili kwa mafanikio dhidi ya hatua hizo zisizo za kibinadamu na zisizo halali kwa zaidi ya miaka 60. Sera ya chuki ya Washington dhidi ya Havana imekosolewa na taasisi mbalimbali za kimataifa.

Tangu mwaka 1992, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limekuwa likipiga kura kila mwaka kuhusu azimio la Cuba la kutaka kuondolewa kwa vikwazo vya Marekani.

Kila mara azimio hilo linapowasilishwa, serikali ya Cuba hutaja vikwazo vya muda mrefu vya Marekani kama chanzo cha matatizo ya kiuchumi nchini humo, ikiwemo uhaba wa bidhaa. Serikali ya Cuba huviita vikwazo hivyo kuwa “vita ya kiuchumi.”

Katika miongo ya hivi karibuni, Umoja wa Mataifa umetoa maazimio kadhaa ukitaka Marekani kusitisha vikwazo na mzingiro wa kiuchumi dhidi ya Cuba, lakini Marekani imeendelea kupuuza kikamilifu wito huo wa kimataifa na kusisitiza kuendeleza shinikizo dhidi ya Cuba.

Baadhi ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa, katika ripoti ya Agosti 2020, walikosoa vikwazo vya Marekani dhidi ya raia wa Cuba wakati wa janga la COVID-19, wakisisitiza kuwa vikwazo hivyo, vinavyodaiwa kuwa kwa ajili ya kutetea haki za binadamu, kwa hakika vinaua watu na kuwanyima haki zao za msingi kama vile huduma za afya, chakula na maisha bora. Cuba ilikadiria kuwa kufikia mwaka 2023, vikwazo hivyo vimeisababishia hasara ya dola trilioni 1.34 katika uchumi wake.

Marekani, kwa mujibu wa Kanuni ya Monroe inayotambua Amerika ya Kusini kama eneo la ushawishi wake wa kipekee, imekuwa ikijihusisha mara kwa mara na masuala ya ndani ya nchi za eneo hilo, hasa Cuba, na imeendesha juhudi za muda mrefu za kuangusha serikali ya Havana.

Lengo halisi la Washington kupitia vitisho vya kiuchumi na kifedha dhidi ya Cuba ni kudhoofisha serikali kisasa na hatimaye kuiondoa madarakani.

Hata hivyo, sera hii ya Marekani imekumbwa na upinzani na kulaaniwa kwa kiwango kikubwa duniani na pia katika Amerika ya Kusini. Mwelekeo huu unaashiria hulka ya kiimla na ya kiutawala ya Marekani. Na licha ya juhudi hizo, Cuba imeendelea kwa mafanikio kupinga hatua hizo zisizo za kibinadamu na zisizo halali kwa zaidi ya miongo sita.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *